ALIYEZUSHIWA UJAMBAZI WA DAR MTANDAONI AIBUKA,ATOA TAMKOMfanyabiashara Ashaeri Mollel


Mfanyabiashara wa mjini Arusha aliyetangazwa kupitia mitandao ya kijamii akihusishwa na ujambazi uliotokea Mbagala jijini Dar es Salaam, ameibuka na kukana taarifa hizo na kusema zilisambazwa na washindani wake.

Tukio la majambazi kupora na kuua katika benki ya Access tawi la Mbagala lilitokea Februari 26, mwaka huu na watu kadhaa wanaendelea kushikiliwa na polisi.

Mfanyabiashara huyo, Ashaeri Mollel aliiambia Nipashe kuwa baada ya tukio hilo, washindani wake ambao hata hivyo hakuwataja, waliisambaza picha yake kwenye mitandao ya kijamii wakimhusisha na tukio hilo, hali iliyomsababishia usumbufu kwa familia na marafiki zake.

“Nimekuwa nikipigiwa simu na watu mbalimbali wakiniulizia imekuwaje nikahusika kwenye tukio hilo, sasa inakuwa usumbufu mkubwa na wapo walioathirika kisaikolojia kutokana na uzushi huo,” alisema.

Hata hivyo, Mollel alisema katika siku za karibuni alitofautiana na mfanyabiashara mwenzake (jina tunalo) wakati wakiuziana gari, hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na kuwapeleka kituo cha polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mollel, wakiwa kwenye gari la polisi baadhi ya watu waliwapiga picha zilizosambazwa kwenye mitandao hiyo zikiwa na maelezo potofu kuwa alihusika na tukio la uporaji kwenye benki.

“Ukweli ni kwamba baada ya kufikishana polisi, kila mmoja wetu alitoa maelezo na tukaachiwa huru, lakini cha kushangaza wenzangu wakachukua picha zile na kunizushia kwamba nilihusika kwenye ujambazi wa Mbagala, inasikitisha ,” alisema.

Mollel ameshawasilisha malalamiko yake Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na kutakiwa kuwasilisha maelezo ya awali polisi ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.


CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post