MWANAMKE ALIYEPAMBANA NA MAJAMBAZI NA KUNYAKUA SILAHA AINA YA SMG APEWA ZAWADI NA JESHI LA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Gemini Mushi amemzawadia pesa taslimu kiasi cha shilingi laki 5 (Tsh 500,000) Sophia Manguye mkazi wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara kwa ushujaa wake wa kupambana na Majambazi na kufanikiwa kuwanyang'anya silaha aina ya SMG.

HABARI KUHUSU MWANAMKE HUYU JASIRI

Mwanamke mmoja mjasiriamali, mkazi wa kitongoji cha Burima kata ya Sirari wilayani Tarime, juzi alifanya tendo la kishujaa baada ya kupambana na kuwanyang’anya bunduki aina ya SMG yenye risasi 27 watu watatu wanaosadikika kuwa ni majambazi.
 
 
Watu hao walivamia maduka katika kata ya Sirari na kupora fedha na vocha za simu za mkononi kwenye maduka na vibanda kadhaa, lakini walipofika kwenye kibanda cha Sophia Manguye hali ilikuwa tofauti kwao baada ya kunyang’anywa silaha.
 
 
Kwa mujibu wa Kamanda Polisi Mkoa wa kipolisi wa Tarime/Rorya, Gemini Mushi, majambazi hao walipoingia kwenye kibanda cha Bi. Sophia walifanikiwa kuiba kiasi cha shilingi 80,000 ikiwa ni baada ya kufanikiwa kupata shilingi 100,000 kwenye maduka waliyopita awali.
 
 
Kamanda Mushi alieleza kuwa watu hao hawakuridhika na kiasi hicho cha fedha na kuamua kuingia ndani kutafuta fedha nyingine. Ndipo Bi. Sophia alipomvamia mmoja aliyekuwa na silaha na kumng’angania kwa nguvu huku akipiga kelele hadi wananchi na polisi walipofika katika eneo la tukio.
 
 
Ingawa majambazi hao walimjeruhi kwa vipigo mwanamke huyo, alifanikiwa kutomuachia jambazi mwenye silaha hali iliyopelekea majambazi wengine wawili kukimbia kabla polisi na wananchi hawajafika katika eneo hilo la tukio.
 
 
Kamanda Mushi alimpongeza mwanamke huyo kwa kufanikisha kukamatwa kwa mtu huyo aliyemtaja kwa jina la Gesanta Matinde mwenye umri wa miaka 19, mkazi wakijiji cha Keheyo, kata ya Mbogi, pamoja na bunduki waliyokuwa wakiitumia aina ya SMG namba UK 5115.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post