MSICHANA MTANZANIA AFANYIWA UKATILI HUKO INDIA,APIGWA,AVULISHWA NGUO NA KUTEMBEZWA UCHI MTAANI

Mtanzania anayesoma India amepigwa, kuvuliwa nguo na kisha kulazimishwa kutembea akiwa uchi na kundi la watu nchini humo.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 (jina linahifadhiwa) anayesoma shahada ya biashara, mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Acharya, Bangalore, alifanyiwa ukatili huo akiwa na Watanzania wengine wanne.

Gazeti la Deccan Chronical la Bangalore, liliripoti kuwa tukio hilo lilitokea Januari 31, baada ya mwanafunzi raia wa Sudan, Ismail Mohammed kugonga gari la raia mmoja wa India, mkazi wa Hesaraghatta aliyekuwa na mkewe na kusababisha kifo cha mama huyo.

Nusu saa baadaye, Watanzania watano akiwamo aliyevuliwa nguo, walifika katika eneo hilo wakiwa kwenye gari ndipo kundi la watu hao lilipoanza kumshambulia binti huyo, kisha kumvua nguo na kumlazimisha atembee uchi.

Baada ya kuchoma gari lililosababisha ajali hiyo, kundi hilo pia liliteketeza gari alilokuwamo Mtanzania huyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mindi Kasiga alisema Balozi wa Tanzania nchini humo, John Kijazi ameshakutana na wanafunzi hao na ameshazungumza na Serikali ya India kuhusu tukio hilo.

Gazeti la Deccan Chronical liliripoti kuwa licha ya polisi waliokuwapo eneo hilo hawakuchukua hatua yoyote hata pale msamaria mwema aliyejitokeza kumsitiri msichana huyo kwa fulana yake ambaye pia alipigwa huku fulana hiyo ikichanwa.

Mshauri wa masuala ya sheria kwa wanafunzi kutoka Afrika wanaosoma Bangalore, Bosco Kaweesi alinukuliwa na gazeti la The Chronical akisema hata dereva wa gari alilokuwa Mtanzania huyo, Micah Pundugu alipigwa na kujeruhiwa vibaya.

Alisema hata pale msichana huyo alipojaribu kupanda basi ili kujinusuru na zahama hiyo, abiria walimshusha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post