MGONJWA AUA MGANGA WAKE KWA KUMKATA JEMBE




Mganga wa jadi wa Kijiji cha Ididi, Kata ya Nyamilangano wilayani Kahama, Jilumba Mabula (70) ameuawa kwa kupigwa na jembe shavuni akiwa kwenye harakati za kumnywesha dawa mteja wake anayedaiwa kuwa mgonjwa wa akili.

Tukio hilo lilitokea juzi, nyumbani kwa mganga huyo wakati akijaribu kumpa dawa mgonjwa huyo aliyepelekwa kutibiwa ugonjwa huo akitokea Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange alisema baada ya mgonjwa huyo kugoma kunywa dawa, mganga huyo kwa kushirikiana na watu wengine walimshika kwa nguvu na kumwangusha chini, kisha kuanza kumnywesha kwa nguvu.

“Unajua mgonjwa wa akili anapogoma kunywa dawa huwa anashikwa kwa nguvu nyingi na kuanza kumbana mdomo ili ameze. Ndivyo ilivyofanyika kwa mgonjwa huyo ambaye alikuwa amegoma akidai wanampa dawa ya nini wakati haumwi,” alisema.

Nyange alisema mgonjwa huyo alifanikiwa kuwaponyoka na pembeni kulikuwa na jembe ambalo alilichukua na kumpiga nalo mganga huyo shavuni, hivyo kumvunja taya la kulia, hali iliyosababisha kifo chake papo hapo.

Kamanda huyo alisema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na yuko mahabusu maalumu ya wagonjwa wa akili na kwamba, anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Nyamilangano, akiwamo Joseph Maziku walisikitishwa na kifo cha mganga huyo wakisema ni pigo kwa wananchi wengi kwa kuwa alikuwa msaada katika eneo hilo.

Maziku alisema hata yeye alifika kutibiwa kwa mganga huyo akitokea wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

“Imeniumiza sana kwa kweli, maana huyu mzee alikuwa akitusaidia watu wengi katika eneo hili na baadhi ya watu walikuwa wanatoka mbali kuja huku kufuata huduma zake,” alisema.

Magreth Nkera alisema mgonjwa huyo hastahili kushitakiwa kwa kuwa anaumwa.

“Naamini kwamba asingekuwa mgonjwa asingeua,” alisema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post