MANISPAA YA SHINYANGA KUJENGA UKUMBI WA KISASA BAADA YA ULE WA KWANZA KUCHOMWA MOTO KWENYE UCHAGUZI MKUU


Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna akizungumza juzi katika ikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga


Madiwani wa manispaa ya Shinyanga wakiwa ukumbini

Madiwani wakiwa ukumbini

Katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi akizungumza ukumbini
Naibu meya wa manispaa ya Shinyanga Agnes Machibya akizungumza katika kikao cha baraza hilo la madiwani-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
*****

Halmashauri ya manispaa ya Shinyanga inatarajia kuanza kujenga ukumbi wa kiasi cha shilingi milioni 100 ili kuondoa usumbufu kwa madiwani wake ambao wamekuwa wakilazimika kutumia ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga kuendesha vikao vyake.

Awali manispaa hiyo ilikuwa na ukumbi wake ambao pamoja na kwamba ulikuwa mdogo, ulichomwa moto na wananchi wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hivyo tangu mwaka 2011 wamekuwa wakitumia ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Akitoa taarifa kwenye kikao cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo,kilichofanyika juzi katika ofisi ya mkuu wa mkoa,mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna alisema tayari shilingi milioni 5o zimepatikana na kwamba hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu ujenzi huo utakuwa umekamilika.

“Tuna milioni 50 za kuanzia,sasa tunaendelea kutafuta fedha zingine ili kukamilisha ujenzi huu,matarajio yetu baraza la madiwani la mwezi Juni,2016 lifanyike kwenye ukumbi wetu”,aliongeza Kalinjuna.

Kwa upande wao madiwani wa manispaa hiyo Hassan Mwendapole na David Nkulila walipongeza jitihada za manispaa hiyo kuwajengea ukumbi kwani tangu mwaka 2011 wamekuwa wakitumia ukumbi ambao uko mbali na ofisi za manispaa hiyo na kusababisha kero kwa madiwani.

Naye Katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi aliwataka madiwani hao kutanguliza mbele maslahi ya wananchi badala ya kuendeleza mvutano wa kisiasa kwenye vikao kwani serikali ya awamu ya tano haihitaji mambo hayo na badala yake wachape kazi ili kutekeleza kauli mbiu ya “Hapa Kazi tu”.
 
 Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527