JINSI KIGOGO WA BODI YA MIKOPO ALIVYOTUMBULIWA JIPU BILA GANZI NA WAZIRI WA ELIMU



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), George Nyatage kutokana na kuwepo na ukiukaji wa utoaji wa mikopo pamoja na ucheleweshaji usio kuwa na sababu za msingi.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Profesa Ndalichako amesema kuwa bodi ya mikopo imekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanafunzi wanaostahili kupata mikopo na kufanya kwao kuweza kupata mikopo mpaka waandamane wizarani kwa kusababishwa na watu wachache wa bodi hiyo.


Kutokana na udhaifu wa kiutendaji wa bodi hiyo baada ya kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji, watendaji watatu wa bodi hiyo wamesimamishwa kazi ambao ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Juma Chagonja pamoja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo, Onesmo Laizer.


Profesa Ndalichako, amesema katika udhaifu wa utendaji huo ni pamoja na ulipaji wa mikopo kwa wanafunzi 23 waliolipwa katika vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu mfululizo kwa chuo cha kwanza zililipwa zaidi ya sh.milioni 653 na chuo cha pili ni zaidi ya sh. milioni 147.


Amesema baadhi ya wanafunzi ambao walikwenda kusoma nchini Algeria wamekuwa wakiendelea kulipwa fedha wakati mkataba wao umekwisha kwa kipindi cha miaka saba.


Profesa Ndalichako amesema wanafunzi 169 walipata mikopo katika vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu mfululizo na kulipa chuo cha kwanza zaidi ya sh.milioni 658 na chuo cha pili zaidi ya sh. milioni 665 na wanafunzi 55 walioacha masomo walilipwa zaidi ya sh.milioni 136 huku wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika walilipwa zaidi ya sh.milioni 342.


Aliongeza kuwa zaidi ya sh.milioni 159 zililipwa kwa wanafunzi 306 zaidi ya kiwango kilichobainishwa kutokana na muongozo wa upangaji na ukopeshaji wa mwaka 2008/2009 na 2009/2010.


Aidha amesema kuwa wanafunzi 77 walipatiwa mikopo kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja ambapo walilipwa zaidi ya sh.milioni 467 kwa vyuo nje na zaidi ya sh.milioni 123 kwa vyuo ndani pamoja na wanafunzi 19,348 walipata mikopo bila kupitiwa na kamati ya mikopo jambo ambalo ni kinyume na kanuni na 8ya kanuni za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.


Hatahivyo amesema wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuwa wameomba ambapo walilipwa zaidi y ash.milioni 207 ambazo zilipelekwa kwenye vyuo sita.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527