ACACIA STAND UNITED FC KESHO KUWEKA KAMBI NZITO MGODINI KUWAKABILI MAAFANDE WA JKT RUVU




Timu ya Acacia Stand United Fc (CHAMA LA WANA) inayodhaminiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Dhahabu ya ACACIA,mara baada ya kupoteza mchezo wake wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kufungwa goli 2-1 na Simba Sc,kesho Jumatatu inatarajia kuingia kambini katika Mgodi wa Dhahabu BUZWAGI kujiandaa na mchezo wake unaofuata dhidi ya Maafande wa jeshi la kujenga taifa JKT Ruvu.

Afisa habari wa klabu hiyo Isaac Edward amesema kupoteza mchezo wao dhidi ya Simba Sc ni sehemu ya matokeo ya Mpira wa miguu, kwani hivi sasa ligi ni ngumu na kila timu inapambana ili kupata matokeo mazuri.


“Tumepoteza mchezo wetu tukiwa nyumbani dhidi ya Simba ni sehemu ya mchezo,tunajipanga na mchezo unaofuata nyumbani ambao tutacheza na Jkt Ruvu , timu inatarajia kuingia kambini siku ya kesho Jumatatu katika Hosteli za Mgodi wa Dhahabu BUZWAGI kujiandaa na mchezo wetu unaofata”

Ameongeza kuwa mchezo ujao timu hiyo ya Acacia Stand United imejipanga kuhakikisha inapata ushindi ili wazidi kujiweka sehemu nzuri kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara.

“Uongozi pamoja na Benchi la Ufundi tumejipanga vilivyo ili tupate pointi tatu ambazo zitazidi kutuweka katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi ” ,ameleeza.

Edward amewaomba mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kuunganisha nguvu kwa pamoja na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri nyumbani na Ugenini.


“ Mashabiki wetu na wapenzi wa Acacia Stand United (Chama la wana) waendelee kuipa timu ushirikiano katika michezo yetu yote iliyobaki katika mzunguko wa pili ambao ni wa lala salama ikiwa tunacheza nyumbani na hata ugenini pia ”,ameongeza.


Acacia Stand United Fc kwa sasa imejikusanyia pointi 29 katika michezo yake 18 walioshuka dimbani katika msimu huu wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527