SAKATA LA KIJANA KUDAIWA KUFIA MAHABUSU SHINYANGA-JESHI LA POLISI LATOA TAARIFA KAMILI



Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Mika Nyange akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake-picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga


Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Mika Nyange

Kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Ndatulu Sangaya(33) amefariki dunia muda mfupi baada ya kupewa dhamana katika mahakama ya Mwanzo Mwamashele wilayani Kishapu mkoani Shinyangakwa kosa la shambulio la kudhuru mwili wa mmoja wa wananchi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Mika Nyange tukio hilo limetokea Januari 15,2016 katika eneo la Mwamashele tarafa ya Ukenyenge wilayani Kishapu.

Akielezea tukio hilo Kamanda Nyange alisema Ndatulu Sangaya ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ipembe wialya ya Igungamkoani Tabora ,kabla ya umauti kumfika alikuwa katika chumba cha mahabusu ya Mahakama ya Mwanzo Mwamashele alipokuwa amehifadhiwa kwa kosa la shambulio la kudhuru mwili wa mmoja wa wananchi katika eneo hilo.

“Huko Mahabusu alikuwa na baba yake mzazi Sangaya Shishi(78) mkazi wa kijiji cha Ipembe wilayani Igunga,wote walikamatwa na kupelekwa katika rokapu ya mahakama ya Mwanzo Mwamashele kwa shtaka la shambulio la kudhuru mwili,wakati mahakama inafanya jitihada za kuwapatia dhamana marehemu alionekana kuwa anaumwa”,alieleza Kamanda Nyange.

“Hakufariki ndani ya chumba cha mahabusu,wakati utaratibu wa kumpeleka katika zahanati ya Mwamashele ili apatiwe matibabu ndiyo akafariki dunia na uchunguzi wa daktari ulionesha kuwa Ndatulu Sangaya alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya mwili na kusababisha kifo chake”,aliongeza Kamanda Nyange.

Kamanda Nyange alisema tukio hilo lilivuta hisia kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kutokana na kifo hicho ndipo jeshi la polisi likafungua kesi ya uchunguzi juu ya kifo hicho na kubaini kuwa Ndatulu Sangaya alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya mwili akiwa rokapu na kusababisha kifo chake.

“Tukio hili lilizua mashaka kwa wananchi,kwani wengine walidai pengine amefariki kutokana kipigo akiwa rokapu lakini niwatoe tu hofu wananchi kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wa daktari kifo chake kimetokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua ”,alisema kamanda Nyange.

Hata hivyo Nyange alisema bado jeshi la polisi mkoani Shinyanga linaendelea kufanya uchunguzi wa tukio la kifo hicho. 
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527