Makala!! ELIMU YETU NA SARAKASI ZAKE

Nilicheka sanaaaa baada ya kusikia, lakini baadaye baada ya kumaliza kucheka ghafla si nikawa nasikitika pekee yangu halafu nikawaangalia wanangu na kisha nikaitazama picha ya bwana mkubwa yule pale wa magogoni nikakumbuka ahadi zake wakati wa kampeni za kuwania “Unyerere” na mwisho nikaangalia kasi yake katika siku hizi chache alizokaa pale kiwanja namba moja nikawa naona kizunguzungu kama siyo kihindi hindi.


Baada ya kuingia madarakani kasi ya awamu ya tano “majipu” yanayotumbuliwa, kuteuliwa baraza la mawaziri, kuteuliwa kwa makatibu wakuu nk vyote vikamalizika na sasa kazi inaendelea kufanyika,kodi inakusanywa ya kutosha, majipu yanatumbuliwa na kila mtanzania anasema la kwake wapo wanaokosoa,wapo wanaopongeza lakini wapo ambao wapo wapo tu si kupongeza wala si kukosoa, ndiyo watasema nini? Walichokuwa wanakitaka wamekipata..!

Sasa bwana kaka mkubwa kilichonifanya nicheke, nisikitike na kuwaza yote ni hapa majuzi wakati Yule Mama yetu aliyeteuliwa kuwa kiranja mkuu wa Elimu alipotembelea ile nyumba ambayo ndiyo ofisi za hawa wakubwa wa Elimu yetu wanamofanyia shughuli zao za kila siku za kutafuta mkate wa kuwapelekea wana familia nyumbani.

Baada ya kufika hapo akapiga nao “stori” mbili, tatu ghafla si akataka kujua huu mpango wao wa viwango vya kufaulu upoje? Kwanini wameweka? Utatusaidiaje? Basi bwana aliyeulizwa swali si akaanza kujibu kana kwamba ameamka usingizini halafu haelewi kinachoendelea, Mama Dada mkuu wa Elimu alivyoona vile si akawapa siku 7 wampe majibu nini faida ya madaraja hayo yanayolingana na viwango vya ufaulu katika Vyuo vikuu na vyuo vya kati, hapo ndiyo nikacheeeka na kuishia kusikitika….! Hahahaahah nchi hii bwana..??

Hivi kumbe mkipewa nafasi tuuya kusimamia jambo Fulani kwa niaba ya Watanzania wenzako tu lazima uanze kupangua pangua vitu kana kwamba unapanga vyombo kabatini? Eeh? Nawauliza ninyi hapo muliopewa dhamana kwa niaba yetu mnajipangia kwa kuwa ninyi mlishasoma mpaka viwango vya udaktari na uprofesa mnaona basi na wenzenu wasifikie huko ulikofikia kwa kuanza kupangua pangua vitu?? Alaa hayo siyo mambo hayo kaka nishasema sasa acheni hizo…khaaa!

Kwanza ebu tujiulize, nini kipaumbele kwenye elimu yetu, je ni madarasa?madawati? wanafunzi? Maabara? Madaftari? Walimu? vitendea kazi au nini? Eeeh maana tukijua sasa ndiyo tunasema ebu tuanze na hili, tuje na hili, kisha tumalizie hili..! Sasa tunapangaje viwango vya ufaulu wakati hatuna madarasa? Tunapangaje wakati walimu wana madeni wamekata tamaa hao? Tunapangaje wakati kuna watoto watoro mashuleni? Tunapangaje wakati kuna watoto wanaachishwa shule kusudi waolewe? Yaani hivi hatuvioni?? Kaka anauliza hatuvioni??

Maana hii Wizara kila anayepewa nafasi basi oooh hiki marufuku fanyeni hivi.! Heee maana namkumbuka Bwana mkubwa mmoja yeye alivyopewa tuu mara oooh hakuna mambo ya michezo mashuleni si shule ya msingi wala nini..! watu haaaa unasemaje wewe? Anasema ndiyo nishasema hivyo matokeo yake watoto wetu kila siku wanachora mazombi tuu katika mitihani kumbe wafanye nini wakati hawana cha kufanya ili kuchangamsha akili zao? Maana hao hao wanaojiita wasomi wanasema michezo hujenga akili ya mwanafunzi sasa ninyi mbona mlifuta??

Sasa bwana kaka mkubwa anasema amechoka kusikia haya mambo na Watanzania pia wamechoka kusikia haya mambo hapa cha msingi tukubaliane katika elimu tunataka hiki na hiki na hiki yaani tunataka Majengo bora,madawati,maabara,walimu walipwe vizuri stahiki zao hivyo viwango vitakuja vyenyewe nakuambia..! ndiyoo.! Unatakaje viwango wakati Mwalimu anawaza kuuza visheti shuleni badala ya kuwaza somo la siku husika? Anawaza visheti vyake kwa kuwa anaidai serikali mihela mingi tu na serikali walaa haisikii kilio chake, mpeni haki yake Mwalimu wangu jamani hiyo GPA iacheni huko huko vyuoni.

Sasa kaka mkubwa ndiyo nimeshasema na Mama yetu Yule Dada wa Wizara amesema amewapa siku 7 mje na majibu msipokuja nayo hatutawaelewa tutawaona na ninyi wale wale tuu aisee…! Kaka mkubwa naona nimeshasema na nimeeleweka kazi kwenu kuyasikia na kuyafanyia kazi ngoja nikaendelee na mambo mengine ya kulijenga taifa langu ambalo sasa hivi kijana wetu Mbwana Samata ameshatutoa kimasomaso kwenye “futibolu” sasa je kwa nini tusijidai…??Makala hii imeandaliwa na Emmanuel Msigwa-Malunde1 blog Dar es salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post