Hii Nayo ya Ajabu!! MSAADA WA MBUNGE WA CHADEMA KWA WAJAWAZITO WAKATALIWA HUKO BUKOBA




Baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea misaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali.


Mbunge huyo mwishoni mwa wiki alikuwa akisambaza vifaa tiba katika vituo vya afya na zahanati, lakini wasimamizi walikataa kuvipokea, huku wengine wakikimbia wakidai walipewa maelekezo na viongozi wao kutovipokea.


Katika hali ya kushangaza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Richard Mihayo ambaye alikuwa katika msafara wa mbunge huyo alitoweka ghafla baada ya kufika Kituo cha Afya cha Zamzam, huku Kaimu mganga, Samwel Chaba akigoma kupokea vifaa hivyo.


Baada ya mkurugenzi kutoweka, mbunge huyo alilazimika kutelekeza vifaa hivyo kituoni hapo na kwenda Zahanati ya Kashai ambako Kaimu Msimamizi wa zahanati hiyo, Emmanel Luviga alikubali kuvipokea.


Katika Kituo cha Afya Rwamishenye vifaa hivyo vilipokewa na wauguzi waliogoma kuzungumza suala lolote.


Baada ya kufika Zahanati ya Kagemu, Msimamizi wake Glory Sailo aligoma kupokea vifaa kwa ajili ya mama wajawazito kwa madai ni maelekezo ya viongozi.


Hatua ya viongozi kuweka vikwazo kwenye upokeaji wa vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh3 milioni ililalamikiwa na Lwakatare aliyedai aliandika barua manispaa na kutoa nakala hadi ngazi ya mkoa, lakini Mganga Mkuu wa manispaa hiyo, Dk Hamza Mgula alisema hajui lolote kuhusu suala hilo.


Akizungumzia suala hilo, Mihayo alisema kwa kawaida vifaa vya tiba ni lazima vikaguliwe na mganga mkuu wa manispaa ili kuthibitisha ubora, hivyo haviwezi kupelekwa bila kuthibitishwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527