Ushirikina Simiyu!! MWANAMKE MCHAWI AKUTWA AKIWA UCHI ,AMENASA KAMA POPO JUU YA NYUMBA YA MTU...ADAI ALIACHWA NA DEREVA WAKE





Grace Ndimishinji (36) mkazi wa Lamadi wilayani Busega Mkoani Simiyu, ambaye amekutwa amening'inia kama popo darini nyumbani kwa mtu, ambapo yeye amedai aliachwa na dereva wake kuwa atampitia.

JESHI la Polisi mkoani Simiyu linamshikilia mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Grace Ndimishinji (36) mkazi wa Lamadi wilayani Busega mkoani Simiyu kwa tuhuma za kukutwa akijihusisha na ushirikina katika familia moja kijiji cha Lamadi kwa kuning'inia kama popo kwenye dari jikoni.


Akizungumza na waandishi wa habari  kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Gemini Mushy amesema tukio hilo limekuwa la kipekee kutokea mkoani huko ambapo mwanamke huyo alikutwa uchi wa mnyama Desemba 22,2015 asubuhi kwenye familia ya Yusta Thomas (35) akiwa jikoni amening’inia bila kujitambua.


"Siku ya tukio ,alfajiri, mama wa familia alisikia sauti za watu nje wakinong’onezana…baada ya kuamka alimkuta mama huyo akiwa darini jikoni akiwa amejining’iniza mithili ya popo ndipo akapiga kelele kuomba msaada kwa majirani’’, amesema Kamanda Mushy.


Amesema kufuatia hali hiyo wananchi walimwamuru kushuka akiwa uchi ndipo  askari polisi walifika eneo la tukio na kumvalisha nguo na kwenda naye kituoni kwa mahojiano zaidi.


Kamanda Mushy amesema mtuhumiwa huyo anaendelea kufanyiwa uchunguzi na atafikishwa mahakamani kwa sura ya 18 kwa sheria za Tanzania kujibu tuhuma za kujihusha na ushirikina.


Akisimulia mkasa huo mama mwenye nyumba Yusta Thomas amesema ilikuwa majira ya saa 8 usiku aliposikia sauti za watu wakiitana majina bila kuwajua ni akina nani lakini wakati huo mbwa wao alipobweka watu hao waliacha mazungumzo na kunyamaza hali iliyomchanganya mama huyo hadi alfajiri.


Yusta alisema akiwa na mwanaye wa kikewalibaini uwepo wa watu wakiongea nje hawakutoka na asubuhi yake walipoamka walimkuta mama huyo akiwa jikoni (nyumba ya nyasi) huku akiwa amening’inia na huku akiwaomba wamsamehe kwa kuwa dereva wake amemwambia ashuke pale atampitia.


"Ule mkao wa darini ulitushtua kwa sababu alikuwa amening’inia, yuko uchi na mkononi kabeba kiberiti kisichokuwa na njiti na akisema mnisamehe kuwa hapa dereva kanishusha hapa na kusema atanipitia’’ ,anasimulia Yusta.


Hata hivyo amesema majaribu ya kimiujiza yalikuwa yakijitokeza katika mji wake mara kwa mara lakini siku hiyo ilikuwa ajabu sana hadi wao wanashangaa huyo mama alifuata nini nyumbani hapo.


Mama huyo (Yusta) alipoulizwa  kuwa ni mbinu gani zilizomfanya mama huyo anase nyumbani kwake na utaalamu gani waliotumia kumshusha mama huyo, Yusta alidai kuwa ni maombi pekee kwani tokea usiku huo alipoanza kusikia minong’ono nje alianza kuomba.


Nao baadhi ya majirani wamesema ni tukio la kusikitisha sana na la kipekee hali itakayosababisha hata watumishi kutofika Busega kufanya kazi kwa kuhofia uchawi huku wakiitaka jamii ibadilike na kuachana na imani zilizopitwa na wakati.


Tukio hilo la kuhusiana na imani za ushirikina ni tukio la pili kutokea wilayani Busega ambapo Septemba 3, 2014 huko Bushigwamhala kata ya Kalemela watu wanne wa familia moja walikutwa asubuhi walikilima wakiwa uchi wa mnyama shambani kwao imani kuwa mahindi hayo yatatoa mavuno mengi wakidai walielekezwa na babu yao enzi za uhai wake

Chanzo:Simiyunews blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527