SERIKALI IMEPANGA KUPELEKA SHILINGI BIL 18.77 KILA MWEZI KILA SHULE YA MSINGI NA SEKONDARI




SERIKALI imepanga kupeleka Sh. 18.77 bilioni kila mwezi katika shule za sekondari na msingi kwa ajili ya kugharamia elimu ili kutekeleza dhana ya elimu bure kuanzia Januari, 2016.


Taarifa hiyo ilitolewa Mjini Dodoma jana na Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa elimu bure.


Alianisha fedha zitakazotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia elimu ni pamoja na gharama za mitihani ya kidato cha nne ambazo zitatolewa moja kwa moja na Serikali katika Baraza la Mitihani (Necta).


“Serikali itatoa pia ruzuku ya uendeshaji wa shule Sh. 10,000 kwa shule za msingi na Sh. 25,000 kwa shule za sekondari kwa kila mwanafunzi kwa mwaka.


“Vilevile itatoa Sh. 1,500 kwa siku kwa mwanafunzi kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wanaokaa bweni,” amesema.


Simbachawene amesema pia Serikali itatoa fedha kwa ajili ya fidia ya ada Sh. 20,000 kwa kila mwanafunzi wa shule ya kutwa na Sh. 70,000 kwa mwanafunzi wa sekondari kwa mwaka.


Amesema fedha za ruzuku ya uendeshaji wa shule zitasaidia pia uendeshaji wa shule za hosteli ikiwemo gharama za chakula, mlinzi, mpishi, umeme na maji.


Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri husika kuhakikisha fedha hizo zinafika kwa wakati na zinatumika kwa kazi iliyokusudiwa.


Simbachawene amesema majukumu ya wazazi pamoja na mambo mengine yatakuwa ni kununua sare za shule, vifaa vya kujifunzia, gharama za matibabu, nauli, gharama za chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa na kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wa bweni.


“Natoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa kusimamia utekelezaji wa elimu bila malipo,” amesema.


Aidha, Simbachawene aliziagiza halmashauri na mikoa ambayo haikufanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba kujieleza sababu za kutofanya vizuri.


“Iwapo itathibitika kwamba kuna wahusika walizembea kutimiza majukumu yao wachukuliwe hatua zinazostahili.


“Nawaagiza pia wakurugezi mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kwamba ifikapo Februari 15 mwakani wawe wamekamilisha miundombinu ya shule ili wawewezeshe wanafunzi 12,647 waliosalia kujiunga na elimu ya sekondari wanaenda shule,” amesema.


Simbachawene pia alizitaka kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya kuwachukulia hatua za kisheria watu watakaosababisha wanafunzi kukatisha masomo kwa utoro na mimba pamoja na wale waliooa watoto wa kike.


‘’Tusifanye kazi kwa mazoea, tunatakiwa tuendane na kasi ya Rais John Magufuli ya kufanya kazi kuwasaidia wananchi hasa katika sekta ya elimu,’’ amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527