Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJIO WA NABII WA KIMATAIFA TB JOSHUA WAZUA GUMZO KILA MTAA TANZANIA..AKUTANA NA LOWASSA NA MAGUFULI..ALITABIRI

 
Ujio wa Nabii wa Kimataifa kutoka Nigeria, TB Joshua aliyetua jijini Dar es Salaam jana na kupokewa na Rais mteule wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli na baadaye kwenda kwa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, umeibua gumzo kubwa kuhusiana na matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25.

Nabii huyo wa Kanisa la The Synagogue, Church of All Nations (SCOAN), aliwasili nchini jana jioni kushuhudia kuapishwa kwa Magufuli kesho.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana ikiwa ni muda mfupi baada ya taarifa za kuwasili nchini kwa TB Joshua kusambaa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, baadhi ya wananchi walisema ujio wa Nabii huyo aliyepokewa na Magufuli ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kuapishwa kwa Rais huyo mteule ni ishara kuwa kweli, kuna siku aliwahi kumtabiria ushindi kabla ya kuanza kwa kinyang’anyiro cha kuwania urais.

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Aggrey, mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, aliiambia Nipashe kuwa hapo kabla, aliwahi kusikia Dk. Magufuli ni miongoni mwa wanasiasa waliowahi kutabiriwa mambo mazuri na TB Joshua na hivyo, ujio wake huo ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuapishwa kwake unampa imani kwamba aliyokuwa akiyasikia ni ya kweli tupu.

“Yawezekana wana urafiki mkubwa baina yao… inawezekana ni kweli aliwahi kumtabiria ushindi huu alioupata. Hata hivyo, vyovyote itakavyokuwa sawa tu kwa sababu TB Joshua ni kiongozi mkubwa wa kidini na Magufuli ndiye kiongozi wetu wa awamu ya tano. Muhimu ni kwa Nabii huyu amuombee Magufuli kutimiza yale aliyotuahidi Watanzania wakati wa kampeni za uchaguzi,” alisema mkazi huyo wa Sinza.

Mkazi wa Kigogo Luhanga jijini Dar es Salaam, Salum Mahwata, alisema ni jambo zuri Magufuli kuonekana akiwa karibu na TB Joshua kwani yawezekana hiyo ni dalili kuwa ataendeleza desturi ya kuheshimu viongozi wa kiroho na kufanyia kazi ushauri watakaokuwa wakiutoa kwake kwa maslahi ya taifa. “Labda jambo kubwa la kuzingatia ni kuona kuwa Magufuli atatoa nafasi kwa viongozi wengine pia wa kidini wakiwamo wa hapa nyumbani na tena wa madhehebu mengine ili kuonyesha kuwa wote anawahitaji katika kuliendeleza taifa letu… hili ni jambo zuri,” alisema Mahwata.

Wengine waliowahi kutabiriwa ni Lowassa, ambaye katika picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii mwaka huu, zilionyesha akiwa katika ibada katika kanisa la Nabii huyo.

Kadhalika, gumzo zaidi kuhusiana na ujio huo wa TB Joshua liliongezeka zaidi jioni baada ya picha nyingine kusambazwa kwenye mitandao zikimuonyesha akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ambaye pia alikuwa akiwakilisha Muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Msemaji wa Lowassa, Abubakar Liongo, jana alithibitisha ujio wa TB Joshua kwa Lowassa, alipoongea na Nipashe kwa njia ya simu.
Kama ilivyokuwa kwa taarifa za kuwa na Magufuli, taarifa na picha hizo za TB Joshua na Lowassa pia ziliibua mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii.

Baadhi ya watu waliokuwa wakichangia mijadala hiyo kuhusiana na ujio wa TB Joshua walidai kuwa ni jambo zuri kwani amekuja kusaidia maombi ya kudumisha amani nchini baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

Magufuli anatarajiwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho baada ya kuibuka na ushindi wa asilimia zaidi ya 58.46, akifuatiwa na Lowassa aliyepata asilimia 39.97

UJIO WAKE
Taarifa na picha zilizosambazwa awali jana zilionyesha kuwa Nabii Joshua alipokewa kwenye Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake, Rais Mteule, Dk. Magufuli jana jioni.
Ilieleza kuwa mara baada ya kuwasili, TB Joshua alikwenda moja kwa moja Ikulu na huko alikutana na Rais Jakaya Kikwete anayekaribia kumaliza muda wake.

Inaelezwa kuwa katika salamu zake, TB Joshua alimpongeza Rais Kikwete kwa kufanikisha uchaguzi mkuu uliofanyika kwa uhuru na amani, huku akiondoka madarakani akiwa mtu mwenye furaha.

“TB Joshua alimpongeza Kikwete kwa kumpata Dk. Magufuli kama mrithi wake, akimtaja rais huyo mpya mteule kama Rais wa Tanzania wa baraka na fanaka tele katika awamu hii mpya,” ilisema sehemu ya taarifa iliyoripotiwa jana.

Kadhalika, taarifa hiyo iliambatana na picha zinazomuonyesha TB Joshua akisalimiana na Rais Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaama.
Ilielezwa zaidi kuwa TB Joshua aliwasili nchini na watu 40 ambao wote watashuhudia kuapishwa kwa Dk. Magufuli kesho.

Baadhi ya picha zilimuonyesha Dk. Magufuli akiwa na mkewe, Janeth Magufuli, wakimpokea TB Joshua kwenye uwanja wa ndege na nyingine wakiwa nyumbani kwake (Magufuli).

UTABIRI WA TB JOSHUA
Miezi michache kabla ya kuanza kwa mchakato wa kumsaka mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hasa baada ya Dk. Magufuli kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea urais, picha zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha yeye (Magufuli), mkewe (Janeth Magufuli) na mtoto wao mmoja wa kiume wakiwa kwa Nabii huyo.

Wakati huo, ilielezwa kuwa TB Joshua alimtabiria Dk. Magufuli kuwa siku moja atakuwa Rais wa Tanzania. Hata hivyo, taarifa hizo hazikuthibitishwa wakati huo, kwani wengine waliowahi kuonekana wakiwa kwa TB Joshua ni pamoja na mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyewakilisha pia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa na pia mtia nia mwingine kati ya 38 wa CCM, Mwigulu Nchemba.

Kanisa la TB Joshua la Scoan huendesha kituo cha luninga cha Emmannuel TV, ambacho kimejitwalia umaarufu mkubwa.

TB Joshua amewahi kutunukiwa nishani kama ‘Officer of the Order of the Federal Republic’ (OFR) na serikali ya Nigeria mwaka 2008 na pia aliwahi kuchaguliwa kuwa mtu wa Karne toka kabila la Yoruba nchini Nigeria. Alipewa wadhifa huo na taasisi ijulikanayo kama Pan-Yoruba media outlet Irohin-Odua.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com