Makubwa Haya!! WALIOISHI CHINI YA ARDHI KWA SIKU 41,WAKILA VYURA NA MENDE SASA KUPAKWA VINYESI ILI KUONDOA MIKOSI


Wazee wa kimila wa makabila ya Wakurya na Waluo wamesema watu watano waliookolewa kutoka kwenye machimbo ya Nyangalata, Kahama mkoani Shinyanga ambao waliwekewa matanga kabla ya kuibuka wanatakiwa kufanyiwa mambo ya kimila, vinginevyo watakufa kiajabu.


Mmoja wa wazee hao, Ghati Ryoba (61) wa Mtaa wa Mwangaza, Nyamisangura – Tarime amesema: “Mtu akidaiwa kuwa amekufa lakini baadaye akaonekana, wazee wa ukoo au wa mila humfanyia matambiko kama njia ya kuondoa mikosi kwake na kwa familia yake. Wanachukua kondoo mweusi wanamchinja kisha wanamtambikia (bharamsendola).


“Kisha wanachukua kinyesi cha kondoo (ubhuhu ghwaling’ondi) na mti mmoja unaitwa (richirya) kisha kile kinyesi kinarushwarushwa ndani ya nyumba yake na mji mzima kama kuna nyumba nyingine halafu wanachukua kile kinyesi cha kondoo na kumpaka kwenye mikono na anashikana mikono na watu.”


Mzee huyo wa kimila ameongeza kusema kuwa baada ya hapo atanawa mikono kabla ya kuruhusiwa kula na kujumuika na watu.


Amesema baada ya hapo atanyolewa kisha atakwenda kuoga “... Wengine hupeleka nywele kuzizindika kwenye mlima ambako watu hawalimi.”


Kuhusu Waluo, mzee Peter Odello wa Kitembe, Rorya amesema: “Kama inatokea mtu anadaiwa kufa na watu wakafanya matanga lakini baadaye akaonekana, lazima arudi kijijini wamfanyie matambiko.”


Amesema akirudi, wazee watachinja ng’ombe na watu watakaa tena kama walivyokaa kwenye matanga kwa siku mbili au tatu watu wakila kisha kupewa dawa inayoitwa manyasi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post