KINGUNGE SASA KUZUNGUMZIA UCHAGUZI MKUU WA TANZANIA BAADA YA KUKUSANYA TAARIFA ZA KUTOSHA....



Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru amesema atazungumzia mchakato wa Uchaguzi Mkuu baadaye baada ya kukusanya taarifa za kutosha.


Akizungumza kwa njia ya simu baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni na Dk John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutangazwa mshindi, Kingunge bila kufafanua zaidi alisema: “Nitazungumzia mchakato wa uchaguzi baadaye baada ya kukamilisha kukusanya taarifa.”


Mwanzoni mwa Oktoba, Kingunge ambaye amekuwa kada wa CCM kwa miaka 61 (tangu enzi za TANU), alitangaza kujitoa katika chama hicho akisema hawezi kuendelea kuwa ndani ya chama kinachoendeshwa kwa maslahi binafsi.


Kingunge ambaye amefanya kazi kwa karibu ndani ya CCM na Serikali na marais wa wote wa awamu nne, alidai chama hicho kimepoteza mwelekeo na hakijadili mambo muhimu kama ilivyokuwa zamani.


Pamoja na Kingunge kudai hajiungi na chama kingine chochote cha siasa, alionekana kwenye jukwaa la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa kumnadi mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho aliyeungwa na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa.


Uchaguzi Mkuu ulifanyika Oktoba 25, mwaka huu, na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Dk John Magufuli kuwa mshindi baada ya kupata kura 8,882,935 (asilimia 58.46) na kufuatiwa na Lowassa kura 6,072,848 (asilimia 39.97).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post