
Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake limesimama wakati mgombea urais wa chama cha mapinduzi Dr John Pombe Magufuli alipokuwa akitoa hotuba yake ya kufunga kampeni zake katika jiji hilo huku akidai kuwa rushwa na ufisadi nchini umesababisha kudumaa kwa maendeleo na kuongeza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho huku huduma kwa wananchi wanyonge zikisuasua na kuwataka mafisadi na wala rushwa waliomo ndani ya CCM kuanza kuondoka.
Dr Magufuli ambaye hotuba yake imekuwa ikisimama mara kwa mara kutokana na kushangiliwa na wananchi huku viongozi wa meza kuu akiwemo rais Dr Jakaya Kikwete akilazimika kukiacha kiti chake na kwenda kumpongeza amesema serikali yake haitakuwa na cha kufikiria juu ya kupambana na rushwa na ufisadi.
Pia Dr Magufuli amewahakikishia wafanyabiashara ndogo ndogo kuwatengea maeneo maalum ya biashara lakini kuanzisha barabara maalum zitakazowawezesha wafanyabiashara wa bodaboda kuingia katikakati ya jiji la Dar es Salaam bila bugudha huku mama Janeth Magufuli ambaye ni mke wa Dr Magufuli akasimama mbele ya umati huo mkubwa wa wana Dar es Salaam kumuombea mumewe kura.
Awali kabla ya kumtambulisha Dr Magufuli kwa wapige kura, rais Dr Jakaya Mrisho Kikwete amewahakikishia watanzania juu ya uwepo wa ulinzi na usalama wa kutosha kwa watanzania kabla, wakati na baada ya kupiga kura na kuwataka wananchi kurejea majumbani baada ya kupiga kura kwa kuwa hata mahakama imetafsiri vyema sheria ya mita mia mbili kutoka kituo cha kupigia kura.
Mkutano huo wa kuhitimisha kampeni ya Dr Magufuli katika jiji la Dar es Salaam umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali akiwemo waziri mkuu mstaafu Salim Ahmed Salim na viongozi wengine waandamizi wa chama na serikali.
Social Plugin