WAFUASI 61 WA UKAWA WATIWA MBARONI KWA KUFUNGA BARABARA NA KUWAPOPOA MAWE WANANCHI WALIOKUWA WANATOKA KWA MAGUFULI


JESHI la polisi kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Iringa jana walitumia mabomu ya machozi kuwakamata wafuasi zaidi ya 61 wa chama cha Demokrasia na maendeleo (chadema ) akiwemo mgombea ubunge wao jimbo la Iringa mjini mchungaji Peter Msigwa kwa tuhuma za kumpiga mawe mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) Iringa na wananchi waliokuwa wakitoka katika mkutano wa mgombea Urais wa chama cha mapinduzi (CCM) Dr John Magufuli.


Imeelezwa kuwa wafuasi hao ambao wengi wao ni vijana walikuwa wamekutana katika eneo la kambi ya kampeni ya Chadema iliyopo eneo la Hoteli ya Sambala jirani na kambi ya kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) kwa ajili ya kikao cha ndani toka majira ya mchana na jioni ndipo walipofanya vurugu hizo wakati wananchi wakitoka katika mkutano wa kampeni za mgombea huyo wa Urais wa CCM.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 12;30 jioni baada ya wafuasi hao kufunga barabara kuu ya Iringa –Dodoma na kufanya vurugu hizo kwa kuwarushia mawe wananchi waliokuwa wakitoka katika mkutano wa kampeni za Dr Magufuli uwanja wa Samora.


Amesema kuwa wakati jeshi la polisi likiwa katika mkutano wa mgombea huyo wa Urais wa CCM walipokea taarifa kuwa kuna vijana wa boda boda zaidi ya 150 walikuwa wakijikusanya kuelekea katika eneo hilo la Sambala Lodge na baada ya kufuatilia ndipo walibaini kuwa wanakwenda katika kikao chao cha ndani na kwa kawaida jeshi la polisi halikatazi watu kufanya vikao vyao vya ndani .


“Jeshi la polisi halizuii wanachama wa chama chochote cha siasa kufanya vikao vya ndani kwani ni haki yao ya kisheria na kikatiba,lakini baada ya kikao chao kumalizika vijana hao walitoka nje ya ukumbi huo uliopo kando kando ya barabara na kuanza kufunga barabara na kucheza muziki katikakati ya barabara na kuzuia watumiaji wengine wa barabara

"Baada ya vurugu hizo nilimuagiza mkuu wa FFU kwenda kuwatoa watu hao barabarani ila walipuuza na kuishia kumpiga mawe na baadae kukimbilia kujifungia katika Lodge hiyo ya Sambala eneo ambalo wamefanya kama makao makuu ya Kampeni za Chadema “alisema kamanda Mungi.


Amesema wakati wa vurugu hizo baadhi ya vijana waliumia kwa kuruka ukuta na wengine kwa kuanguka wakati wakijaribu kukwepa kukamatwa na kuwa wale wote waliokamatwa watafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa na kuwa miongoni mwao yumo mgombea ubunge jimbo hilo,Mchungaji Msigwa .


Mbali ya mchangaji Msigwa wengine waliokamatwa kwa tuhuma za vurugu hizo ni pamoja na mgombea udiwani kata ya Gangilonga ambae pia ni mkuu wa kambi hiyo Dady Igogo

Hata hivyo, taarifa iliyotufikia jion hii inaarifu kuwa Mchungaji Msigwa na wafuasi hao 61 wameachiwa kwa dhamana leo.



Chanzo Mpekuzi blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527