MAGUFULI AENDELEA NA KAMPENI ZAKE HUKO IRINGA


Wananchi mkoani Iringa wameitaka serikali ijayo ya awamu ya tano kupunguza gharama za pembejeo za kilimo sambamba na kuhakikisha wataalamu wa kilimo wanakuwa karibu na wananchi ili kufanya tafiti na kubaini magonjwa ya mazao wanayozalisha kuwasaidia kupata mazao mengi hivyo kukuza pato huku maafisa ardhi wabadhirifu wakitakiwa kubadili matendo yao.


Wananchi hao wa mkoani Iringa katika eneo la Ilula ambapo ni maarufu kwa kilimo cha mbogamboga wameyasema hayo wakati wa mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea urais wa CCM Dr John Pombe Magufuli na kuongeza kuwa mazao ya kilimo cha mbogamboga hususani nyanya zinaharibika kutokana na kukosa viwanda vya kusindikia mazao hayo na hivyo kusababisha hasara kwa wakulima.

Akizungumza na wananchi wa maeneo ya Kalenge na Igalula na pia Iringa mjini kwa nyakati tofauti wakati akifanya mikutano ya hadhara ya kampeni za kusaka urais kupitia CCM Dr Magufuli ameahidi kuhakikisha uwepo wa kiwanda cha kusindika mazao ya mbogamboga, kutatua kero ya maji lakini pia kuboresha huduma za bima ya afya ili kumhakikishia mtanzania matibabu pale anapougua hususan mtanzania wa kipato cha chini.

Dr Magufuli ambaye amejipambanua kama kiongozi anayechukia rushwa na ufusadi kwa vitendo lakini kiongozi muwajibikaji kwa faida ya wote amewaambia wakazi hao juu ya dhamira yake ya kutumikia mchana na usiku bila ya kujali wadhifa wake.

Dr Magufuli amehitimisha ziara yake ya kusaka kura kwa wapiga kura wa mkoa wa Iringa ambapo jumanne ya September 29 anatarajiwa kuendelea na kampeni zake mkoani Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527