Mwalimu wa shule ya sekondari Manushi kata ya Kibosho Magharibi mkoani Kilimanjaro Demetus Dustan,amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana saa chache baada ya kutokea ugomvi unaohusishwa na kuchanwa kwa picha ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Mwalimu huyo, Demetus Dustan (33) maarufu kwa jina la Kidule, aliuawa Jumamosi iliyopita usiku na mwili wake kukutwa katika shamba la mtu aliyetajwa kuwa ni Joackim Massawe.
Katika taarifa yake kwa vyomo vya habari,jana kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro Fulgence Ngonyani,alisema mwili wa mwalimu huyo ulikutwa Septemba 12 mwaka huu saa 2:30 usiku huko maeneo ya Kibosho Manushi.
Kamanda huyo alisema kabla ya tukio hilo inadaiwa kuwa mwalimu huyo alikwenda kwenye baa inayomilikiwa na na Teresia Jeremia(32) mkazi wa Kibosho ambako alikunywa pombe na watu wengine.
Alisema wakati akiwa kwenye baa hiyo alikuwa akibishana na Albert John(50) mkazi wa Manushi,hadi kupigana na kuamriwa na watu.
"Inadaiwa kuwa akiwa klabuni, kulitokea ubishani kati yake na mtu mwingine uliotokana na kuchanwa kwa picha ya Lowassa ambao ulikwenda mbali na kusababisha wapigane....waliamuliwa na wateja wengine waliokuwapo na baadaye mwalimu huyo aliondoka kurejea nyumbani na hakuonekana hadi mwili wake ulipookotwa",alisema kamanda.
Kamanda huyo alisema kuwa chanzo cha ugomvi inadaiwa mwalimu huyo alikuwa akilalamika kwanini picha ya mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa Edward Lowassa imechanwa.
Alisema baada ya hapo aliondoka kuelekea nyumbani kwake akiwa ameongozana na mtu aitwaye Verani Ulomi(26) mkulima mkazi wa Manushi.
Aidha Kamanda alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa umechubuka kidogo kwenye mguu wa kulia karibu na goti na shati lake likiwa limechanika sehemu mbalimbali.
Alisema kutokana na tukio hilo jeshi la polisi linawashikilia Ulomi na Teresia kwa mahojiano zaidi huku likimsaka Albert.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC Kwa uchunguzi zaidi.
Na Safina Sarwatt-Moshi
Social Plugin