SAMWELI SITTA AMLIPUA LOWASSA SHINYANGA, ATAKA MDAHALO NAYE ILI KUELEZA UMMA ANAVYOHUSIKA SAKATA LA RICHMOND



Mheshimiwa Lowassa na Samwel Sitta wakikumbatiana kabla ya Lowassa kutimkia Ukawa




Mheshimiwa Samweli Sitta akiwahutubia wakazi wa Shinyanga wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi CCM wilaya ya Shinyanga mjini ambapo alisisitiza kuwa mgombea urais wa UKAWA Edward Lowassa anahusika na sakata la Richmond na utajiri wake haueleweki 

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Mbunge wa Urambo aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta ametaka uandaliwe mdahalo kwenye vyombo vya habari kati yake na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa ili kuuleza umma kuhusu ukweli juu ya kuhusika kwake na kashfa ya Richmond.




Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge wakati Lowassa alipojiuzulu kutokana na sakata hilo aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika katika viwanja vya Shy-com mjini Shinyanga.



Alisema sasa yuko tayari kufanyiwa mdahalo maalumu lili kuusimulia umma kuhusu namna Lowassa anavyohusika na sakata la Richmond na ufisadi wake kwani anavyo vielelezo na ukweli wa kilichomfanya ajiuzuru nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008.


“Anachotuzidi Lowassa ni utajiri tu hana kitu kingine,na utajiri wake haueleweki,katika kura za maoni inakadiriwa alitumia shilingi bilioni 8,na mimi nadhani baadhi ya hizo anadaiwa,ndiyo kisa cha kung’ang’ania hadi kuhama chama ili aendelee kuutafuta urais kwa njia yoyote, na mtu wa namna hiyo ni mtu wa kuogopwa sana”,alisema Sitta.


“Mimi sisemi kwamba Lowassa hatoshi kwa kila kitu,kuna vitu flani anatosha,na rais wa awamu ya pili na ya tatu walimteua wakaona anatosha kuwa waziri,lakini tarehe 25,Oktoba mwaka 2015 hatuchagui waziri tunachagua rais jamani”,aliongeza Sitta.


Alisema rais wa awamu ya nne aliingia mkenge kwani pamoja na watu kumwambia kuwa Lowassa siyo mtu mwadilifu,rais Kikwete kwa huruma yake akaona amjaribu uwaziri mkuu,matokeo yake miaka miwili tu akakiona cha moto kwani hakuona aibu ya kujitajirisha kupitia nafasi yake.



“Nilimpokea bungeni miaka 30 iliyopita wakati huo mimi nimekaa bungeni miaka 10,namfahamu vizuri sana,kama kweli anasema hana hatia sakata la Richmond,naomba wiki ijayo tuwe na mdahalo kwenye vyombo vya habari,Harrison Mwakyembe mimi,yeye na marafiki zake taifa zima litusikilize,tuje na vielelezo aje aseme kuwa hana hatia,asikae analia lia tu wakati ukweli ni tofauti”,aliongeza Sitta.



“Kama Lowassa anaona alionewa sakata la Richmond,mimi ndiyo nilikuwa spika wa bunge la tisa,bunge la viwango lilikuwa linatenda haki,tukateua kamati teule,ikabaini mambo machafu kweli kweli yeye na marafiki zake”,alisema Sitta.



Sitta alisema Chama cha Mapinduzi kilikuwa kimejaa wanachama walio mapandikizi wakiongozwa na Lowassa na rafiki yake Khamis Mgeja sasa wameshajionyesha na sasa kimekuwa chama kizuri kama kilivyokuwa enzi za hayati baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere na kitazidi kuimarika na waliobaki wataendelea kutetea ilani na kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola.



Aliwaomba watanzania kumchagua Dkt John Magufuli kuwa rais kwani huyo Lowassa aliyeazimwa na Ukawa hafai kwani ni mtu wa mbwembwe na visingizio.



Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mtera ambaye pia mjumbe katika kampeni ya uchaguzi ya CCM Livinstone Lusinde aliwataka wananchi kutochagua mamluki wala kiongozi mgonjwa kwani ikulu sio wodi ya wagonjwa (akisema Lowassa bila kutaja ugonjwa anaougua) bali wamchague Dkt Magufuli ambaye rafiki yake mkubwa ni Ilani ya CCM na kazi na si vinginevyo.


Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527