Presha ya Uchaguzi!! MBUNGE WA CCM DANIEL NSANZUGWAKO APOTEZA SIFA KWA KUJAZA FOMU KAZALIWA MWAKA 2015




Mgombea Ubunge Jimbo la Kasulu Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Moses Machali, ameweka pingamizi la uteuzi wa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Nsanzugwanko, kwa madai kuwa hafai kuwa mgombea baada ya kujaza fomu kuwa amezaliwa tarehe 15/08/2015.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10 jioni baada ya wagombea wengine kuona fomu yake kwenye ubao matangazo wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu.

Machali alitoa pingamizi hilo jana kwa Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Fatina Hussein, kwa madai kuwa kutokana na mgombea wa ubunge kupitia CCM, Nsanzugwanko kujaza fomu kuwa alizaliwa tarehe hiyo, mwaka huu, hafai kuwa mgombea.

Kwa mujibu wa Machali, kisheria ni kosa kwa mtu mwenye umri chini ya miaka 21 kugombea nafasi ya ubunge, lakini pia kwa kosa hilo ambalo ni la kisheria ni wazi msimamizi wa uchaguzi anapaswa kutomteua mgombea huyo wa CCM ambaye kwa mujibu wa Machali, Nsanzugwanko ameapa kiapo kinachoonesha umri wake ni siku sita.

Alisema katika mazingira hayo amepoteza sifa za kuteuliwa kuwa mgombea na suala hilo halihitaji mjadala.

Hata hivyo, katika hatua iliyowashangaza wananchi ni pale Mkurugenzi huyo kutaka kubandua fomu hiyo ili abandike nyingine.

Akifafanua kuhusu hatua hiyo, Hussein alisema, juzi majira ya saa 10 jioni alibandika fomu kwenye ubao kama sheria inavyosema na ilionekana Nsanzugwanko alijaza fomu kuwa alizaliwa mwaka 2015.

Fatina alisema baada ya wagombea kubaini kuwa fomu ya mgombea wa CCM imekosewa aliwaambia wachukue fomu za pingamizi.

Mkurugenzi huyo aliwataka wagombea kuwa na amani na utulivu na kwamba fomu zitalindwa na uchaguzi utafanyika kwa haki.

Kwa upande wake CCM Nsanzugwanko alipoulizwa kuhusu tarehe hiyo ya kuzaliwa alijibu kwa kifupi: “ Je wewe unaamini, kwa heri.”
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post