Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha(kushoto) akionesha silaha(bastola),risasi,simu walizokamatwa nazo majambazi walioteka magari huko Kishapu mkoani Shinyanga-Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha akionesha risasi( kati ya 18 zilizokamatwa)
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha akionesha bastola walizokamatwa nazo majambazi walioteka magari ya pamba huko Kishapu
Simu nne zilizokamatwa kwenye begi la majambazi waliokamatwa huko Kishapu
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha akiwa ameshikilia moja ya simu walizokamatwa nazo majambazi walioteka magari huko Kishapu
*******
watu wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa fimbo na mawe na wananchi baada ya kuteka magari kisha kupora simu na fedha kiasi cha shilingi 613,000/= katika eneo la Mawe Mawili kijiji cha Mayanji kata ya Ukenyenge wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Agosti 18,2015 saa sita kasorobo usiku ambapo majambazi saba walitega mawe katika barabara itokayo Kishapu kuelekea Kolandoto katika manispaa ya Shinyanga na kuteka magari mawili yaliyokuwa yamebeba pamba kutoka Kishapu kwenda Kahama.
“Majambazi waliteka magari yenye namba za usajili T.485PLZ aina ya scania lori lenye tela namba T.367 CRA na gari lenye namba za usajili T.552 AGL aina ya Benz lenye tela namba T.808 BHD,wakafanikiwa kupora simu za mkononi nne, na pesa taslimu shilingi 613,000/= kutoka kwa madereva na abiria wa magari hayo”,alieleza Kamanda Kamugisha.
Aliongeza kuwa kufuatia tukio hilo,wananchi, jeshi la jadi sungusungu kwa kushirikina na askari polisi walifanya msako katika vijiji vya Ukenyenge,Mayanji,Ikonongo,Songwa,Buganika,Mwigumbi na Mpumbula na kuwakamata majambazi wawili wakiwa na begi moja lenye vitu vilivyoporwa eneo la tukio.
“Majambazi wawili walikamatwa wakiwa na begi lenye bastola mbili aina ya Browing,moja yenye namba A731307 na nyingine namba zake zimefutwa,magazini 3,risasi 18 na simu 4 zilizoporwa katika eneo la tukio”,aliongeza Kamugisha.
Hata hivyo wananchi walijichukulia sheria mkononi waliwapiga hadi kuwaua majambazi hao kwa kutumia fimbo na mawe na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta majambazi watano waliotoroka.
Alisema miili ya majambazi hao ipo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga
Social Plugin