VURUGU NA VITUKO VYATAWALA MKUTANO WA ACT WAZALENDO SHINYANGA,ZOMEA ZOMEA MWANZO MWISHO,MMOJA ANUSURIKA KUUAWA





Mkutano wa hadhara wa Chama Cha ACT-Wazalendo uliokuwa ukiongozwa na mwenyekiti wa taifa Anna Mugwira leo jioni katika Viwanja vya Shycom Mjini Shinyanga umegubikwa na vituko na zomea zomea za hapa na pale baada ya viongozi wa Chama hicho kupanda jukwaani kuwahutubia wakazi wa Shinyanga.

Vurugu hizo zimeanza baada ya katibu mwenezi wa ACT Wazalendo taifa Sabini Richard kupanda jukwaani na kuwatangazia wananchi kuwa kiongozi wa taifa wa Chama Hicho Zitto Kabwe hatahudhuria mkutano kutokana na kuwa na kazi zingine za kichama.


Kufuatia taarifa hizo wananchi walianza kupiga kelele na kuondoka kwenye mkutano huo huku wakilalamika kuwa kwanini chama hicho kiliwatangazia kuwa Zitto atakuwepo kwenye mkutano huo.

Hata hivyo hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya mwenyekiti wa chama hicho taifa Anna Mugwira kupanda jukwaani na kuwakaribisha baadhi ya madiwani waliokuwa wa Chadema katika manispaa ya Shinyanga Nyangaki Shilungushela na Siri Yasin ambapo wananchi walianza kunyosha vidole vya ishara ya Chadema na kuimba Yuda Yuda Yuda!!

Wananchi hao walisikika wakisema kuwa madiwani waliohamia ACT Wazalendo ni wasaliti wa Chadema na hawajafanya lolote katika kata zao wakati wa uongozi wao.


Akizungumza katika mkutano huo huku akizomewa na wananchi Aliyekuwa diwani wa viti maalum kata ya Chamaguha Siri Yasin amesema lengo la ACT wazalendo ni kuwakomboa wananchi na kwamba watakijenga chama hicho kama walivyofanya kazi ya Kujenga Chadema na kuifanya ikue katika manispaa ya Shinyanga.

Yasin amesema waliofanya vurugu hizo wameowaonea wivu madiwani hao wa Chadema waliohamia ACT Wazalendo.

Naye aliyekuwa diwani wa kata ya Kambarage Nyangaki Shilungushela akizungumza katika mkutano huo amewataka wananchi kuwapuuza wanaobeza ACT Wazalendo na kudai kuwa hata wakati wanaianzisha CHADEMA walionekana kupuuzwa na baadaye wananchi kuona chama kinafaa.


Kwa upande wake mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Shinyanga mjini Godwin Makomba amewataka wananchi kuacha kufanya vurugu na kuunga mkono chama hicho.

Awali wakati mkutano unaanza kijana mmoja ambaye hakujulikana jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 25 alinusurika kuuawa na wananchi waliohudhuria mkutano huo kwa madai kuwa alikuwa anaiba pesa za mmoja wa wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Hata hivyo walinzi wa ACT Wazalendo wakishirikiana na askari wa jeshi la polisi walifanikiwa kunusuru maisha ya kijana huyo kisha mkutano kuendelea huku zomea zomea kwa kila kiongozi aliyepanda jukwaani zikitawala hadi mkutano ulipomalizika .


Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa zomea zome hizo zimefanywa na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CHADEMA,huku ikidaiwa kuwa hata huyo kijana aliyenusurika kuuawa ni mpango wa watu hao kuharibu mkutano wa ACT Wazalendo.

Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde,alikuwepo eneo la tukio,ametuletea picha kutoka eneo la tukio,TAZAMA HAPA CHINI



Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Shinyanga mjini Godwin Makomba alifungua mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga

Viongozi wa ACT Wazalendo wakiwasukuma wananchi waliokuwa na hasira,waliokuwa wanamshushia kipigo kijana(yupo hapo chini) aliyedaiwa kuwa alikuwa anaiba pesa kwenye mfuko wa suruali ya mmoja wa wananchi walikuwa kwenye mkutano huo
Kijana aliyenusurika kuuawa baada ya kudaiwa kuiba pesa kwenye mkutano

Wafuasi wa ACT Wazalendo wakimwokoa kijana huyo,yuko chini

Baunsa wa ACT Wazalendo akimwokoa kijana huyo kabla ya askari hawajafika eneo la tukio

Askari polisi akimwokoa kijana huyo

Kijana akiondolewa eneo la tukio na wasamaria wema na askari polisi

Askari polisi wakiwa na kijana aliyenusurika kifo na wananchi wenye hasira

Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo taifa Sabin  Richard akizungumza kwenye mkutano huo na baada ya kusema Zitto Kabwe wananchi wakaanza kupiga kelele(kuzomea) kisha kuanza kutawanyika
Wananchi wakiondoka kwenye mkutano


Katibu mwenezi wa ACT Wazalendo Sabin Richard akiwahutubia baadhi ya wananchi waliobaki kwenye mkutano
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mugwira,akimtambulisha aliyekuwa diwani wa CHADEMA kata ya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga Nyangaki Shilungushela,aliyeambulia kuzomewa na wananchi



Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mugwira,akimtambulisha aliyekuwa diwani wa viti maalum CHADEMA kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga,ambaye pia alizomewa


Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mugwira,akiwahutubia wakazi wa Shinyanga katika wakati mgumu kwani zomea zomea zilitawala

Nyangaki Shilungushela akizungumza katika mkutano huo,huku akieleza kutokereka na zomea zomea hizo akidai kuwa hata wakati wanaianzisha CHADEMA walipuuzwa sana


Baadhi ya wananchi waliokuwa wanazomea wakiwa wamenyoosha vidole viwili wakiimba YUDA YUDA YUDA!!

Siri Yasin akizungumza katika mkutano huo


Zomea zomea na vidole viwili ikiendelea

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527