MHESHIMIWA LOWASSA KESHO KUTUA SHINYANGA

Edward Lowassa
 Khamis Mgeja

Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Hisani kati ya wakongwe (maveterani) wa soka  wa  Timu ya Simba na Yanga kwa ajili ya kupata pesa kusaidia watoto wenye ulemavu wa ngozi(albino) katika kituo cha Buhangija kilichopo katika manispaa ya Shinyanga.
 
Mchezo huo umeandaliwa na taasisi ya Mzalendo Foundation nchini inayojihusisha na Utawala Bora,Haki za binadamu,utamaduni na michezo utafanyika kesho ,Alhamis ,Juni 11,2015 katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga kuanzia saa 10 jioni. 

Mwenyekiti wa taasisi hiyo Khamis Mgeja ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga amesema maandalizi ya mchezo huo yameshakamilika na kuwataka wakazi wa Shinyanga na nje ya mkoa huo kujitokeza kushuhudia mpambano huo na kuchangia watoto wenye ulemavu wa Buhangija.

“Tumemuomba ndugu yetu Lowassa kuwa mgeni rasmi na amekubali kuhudhuria,atakabidhi ngao kwa mshindi,hili zoezi litakuwa la wazi hakuna usiri mapato yatakayopatikana ni kwa ajili ya kusaidia watoto albino”,ameongeza.

Aidha amesema mchezo huo utakuwa wa amani kulaani mauaji ya albino na vyombo mbalimbali vya usalama vitakuwepo hivyo kuwataka watanzania kujitokeza katika mchezo huo wa kuchangia watoto wenye ulemavu wa ngozi wanaolelewa katika kituo cha Buhangija.

Amesema wameamua kuandaa mchezo huo wa magwiji wa soka kwa ajili ya kutafuta pesa kwa ajili ya kuwasadia watoto wanaolelewa katika kituo cha Buhangija wanaoishi maisha magumu wakikabiliwa na changamoto nyingi kubwa zaidi ikiwa ni Chakula.

“Mzalendo Foundation inalaani vitendo vya kikatili dhidi ya albino vinavyoendelea nchini hasa kanda ya ziwa ,katika mchezo huo wa hisani,hapatakuwa na kiingilio chochote bali,mtu mwenye mapenzi mema na watoto hao,atatakiwa kuja na mchango wa angalau kuanzia shilingi 1000/= tu na kuendelea kama sehemu ya mchango kwa mahitaji ya watoto hao”,amesema Mgeja.

Katika hatua nyingine Mgeja ameiomba serikali kupitia wizara zake kuangalia namna ya kusaidia watoto albino ikiwemo kutenga bajeti huku akiwataka wabunge kuweka mkazo katika mambo yanayohusu walemavu wa ngozi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Soka mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) Benester Lugola amesema tayari wachezaji wa timu zote wameshawasili mjini Shinyanga kwa ajili ya mchezo huo.

Amesema  katika mchezo huo hapatakuwa na kiingilio bali yeyote atakayeguswa na hali ngumu ya maisha ya watoto hao anaweza kutoa chochote anachoona kinawafaa watoto hao. 

Kituo cha watoto wenye ulemavu cha Buhangija hivi sasa kina jumla ya watoto 396 kati yao albino 292,wasiiona 40 na wasiosikia 64 na kutokana na ongezeko la albino kwa hofu ya kuuawa changamoto kubwa ni chakula.

Mahitaji mengine kwa watoto hao ni magodoro,vyandarua,vitanda,mavazi na mafuta maalumu kwa walemavu wa ngozi.

 Na Kadama Malunde- Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post