BUNGE LAPITISHA BAJETI KUU YA SERIKALI KWA MWAKA 2015/2016 KWA ASILIMIA 83


BUNGE  limepitisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2015/16 kwa asilimia 83.

Bajeti hiyo, imepitishwa leo mchana mjini Dodoma, baada ya wabunge kuipigia kura kwa kuitwa majina mmoja baada ya mwingine.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alisema wakati upigaji kura unaanza, Bunge lilikuwa na wabunge 262, lakini walipokuwa wakiendelea  idadi iliongezeka kutoka idadi hiyo hadi kufikia 294.

Kutokana na idadi hiyo, alisema wabunge waliopiga kura ya ndiyo ni 219 na walioikataa ni wabunge 74.

Pamoja na idadi hiyo, alisema mbunge mmoja alitoa kauli iliyoonyesha hakushiriki kupiga kupiga kura.

“Wakati Bunge linaanza kupiga kura, ukumbini kulikuwa na wabunge 263,baadaye waliongezeka na kufikia 294.

“Wabunge 59 hawakupiga kura na waliopiga kura ya hapana ni 59,waliopiga kura ya ndiyo ni wabunge 219 ambao ni sawa na asilimia 83.

“Pamoja na takwimu hizi, mbunge mmoja alisema ni abstain kwa maana kwamba hakukubali wala kuikataa bajeti,” alisema Dk. Kashilila ingawa hakumtaja mbunge huyo.
 
Lakini taarifa zinaonyesha ni Mbunge wa Mpanda Mjini,Said Amour Arfi (Chadema).

Pamoja na matokeo hayo, kivutio kikubwa bungeni kilikuwa ni Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) kuikataa bajeti kuu ya Serikali kwa mara ya kwanza tangu Bunge la 10 lilipoanza mwaka 2010.

Kitendo hicho cha Mrema ambacho hakikutarajiwa, kiliamsha shangwe kutoka kwa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa kuwa waliamini angeendelea kuiunga mkono kama alivyofanya kwa miaka minne iliyopita.

Pamoja na Mrema, wabunge wengine waliosababisha kelele za shangwe bungeni kutoka kwa wabunge wa CCM baada ya kupiga kura ya ndiyo ni Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP).

Wakati bajeti hiyo ikipitishwa, baadhi ya wabunge wa upinzani walionyesha kutoridhishwa nayo kwa kile walichosema kuwa haina jipya kwa vile haiwalengi wananchi.

Akitoa maoni yake kwa waandishi wa habari, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema bajeti hiyo ilipita kwa sababu kuna wabunge wengi wa CCM.
 
Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja  ya wananchi kuwachague kwa wingi wagombea wa upinzani, wakati wa uchaguzi mkuu ili Bunge lijalo lisitawaliwe na chama kimoja kama ilivyo sasa.

Naye Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, kama alivyosema Mbowe, naye hakuonyesha kuridhishwa na bajeti hiyo kwa kile alichosema haitaweza kutekelezwa mwaka huu kutokana na uwepo wa uchaguzi mkuu.

Awali akitoa ufafanuzi wa hoja za wabunge walizozitoa wakati wanachangia bajeti hiyo iliyowasilishwa wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alizungumzia tozo ya Sh 100 iliyopendekezwa na Serikali katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Kwa mujibu wa Mkuya, Serikali inatarajia kukusanya Sh bilioni 276 kutokana na tozo hiyo na kwamba fedha zitakazopatikana zitapelekwa kwenye miradi ya umeme vijijini na katika miradi ya maji.

“Lengo la Serikali ni kuwapelekea wananchi umeme katika maeneo yao na ndiyo maana tumeona ni bora wachangie shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta hayo.

“Kwa kuwa lengo letu ni hilo, wenzetu wasiifanye kama hoja ya kujiongezea umaarufu kwa sababu Sh bilioni 276, zitakapopatikana, Sh bilioni 90, zitapelekewa kwenye miradi ya maji na zitakazobaki zitapelekewa kwenye miradi ya umeme,” alisema Mkuya.
 
Kuhusu malipo ya pensheni kwa wastaafu, alisema Serikali imeyaongeza kutoka 50,000 walizokuwa wakilipwa kwa mwezi hadi Sh 100,000.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post