URAIS NDANI YA CCM NOMA,HOFU YATANDA MPANGO WA KUIVURUGA KAMATI KUU KABLA YA KUCHUJA MAJINA YA MAKADA WANAOUTAKA URAIS

Mbio za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu. 

Hadi sasa CCM haijatangaza ratiba yake kwa ajili ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.
 
Hata hivyo, Mwananchi ilitaarifiwa wiki hii kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 21 na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kikongwe.
 
Wakati chama kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja ya makundi ya makada wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo wa Kamati Kuu ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka majina Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
 
Taarifa ambazo Mwananchi limezipata zinaeleza kuwa kundi hilo linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura ya kutokuwa na imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea baadhi ya waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
 
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa kundi hilo limekuwa likifanya vikao mbalimbali vya kuweka mkakati wa jinsi gani ya kuivuruga Kamati Kuu kabla ya kuchuja majina ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM.
 
“Kuna mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa kuwa ukishapita hapo, umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani ya chama na kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi kukipigania chama na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika serikali ijayo,” alisema mpashaji habari wetu ambaye ni mmoja wa viongozi wa juu wa CCM.
 
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mpango huo unafanyika kwa umakini mkubwa ili kuweza kuhakikisha Kamati Kuu haikati jina la mgombea wa kundi hilo kama ambavyo imewahi kufanyika kwa makada wengine ambao majina yao hayakupelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura kutokana na nguvu yao kwenye chama.
 
Kama hilo litafanikiwa itakuwa ni kwa mara ya pili kutokea baada ya mwaka 1995, Jakaya Kikwete kumlalamikia aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Lawrance Gama kuwa hawezi kumtendea haki baada ya kuonekana akiwa amevaa nguo yenye nembo ya mmoja wa waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais.
 
Alipoulizwa kuhusu mkakati huo, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa wamesikia na kuelezwa kuwa kundi hilo linagawa fedha kufanikisha jambo hilo kwa kuwa wanadhani sekretarieti ya chama haiwapendelei wao.
 
Wanadhani kuna watu wanapendelewa, kama suala hilo lipo bila shaka chama hakiwezi kukaa kimya kwani huo ni uasi na usaliti kwa chama,”alisema Nape.
 

Alisema kuwa ndani ya chama viko vyombo vingi ambavyo kama mtu ana shida anaingia kwenye mikutano sahihi ya chama.

“Mtu huwezi kutengeneza vikao nje ya vikao halali halafu urudi kuongoza chama hicho hicho,” alisema Nape.
 
“Labda watu wana mpango wa kukivuruga chama hiki halafu wagombee kwa chama kingine sawa, lakini kama wanataka kugombea humuhumu CCM, haitawezekana,” alisema Nape.
 
Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye pia ni Meya wa Ilala, Jerry Silaa alipoulizwa kuhusu mkakati huo kama amesikia, hakuwa tayari kusema chochote kwa kuwa yeye yupo ndani ya Kamati Kuu.
 
Hadi sasa makada sita wa CCM wamefungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kujishirikisha na harakati za uchaguzi ndani ya chama. Makada hao ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Pia, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
 
Baadhi ya makada wanaotajwa kutaka urais kwa tiketi ya chama hicho ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, waziri wa zamani wa Ulinzi, Emmanuel Nchimbi, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli.
 
Alipoulizwa kama kuna watu wanapita kushawishi wanachama kujiunga na mkakati huo, mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alisema hofu hiyo inatokana na chama kuchelewa kuruhusu wanachama wake kuingia kwenye mchakato.
 
“Kama chama kingeruhusu mapema, kingedhibiti mapema mambo haya,” alisema Mgeja.
 
Muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo, Mgeja, ambaye anaingia kwenye vikao vya Halmashauri Kuu ya CCM kutokana na nafasi yake kwenye mkoa, alipiga simu na kumweleza mwandishi kuwa anataka kuwatoa hofu wanachama wa CCM kuwa chama kiko imara na hakuna ajenda ya mpasuko ndani ya chama.
 
Akizungumza na gazeti la Mwananchi kwa simu, Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumburi, alisema amesikia kuwapo kwa mpango huo lakini hajathibitisha.
 
“Hata mimi nimezisikia habari hizo ingawa hazijathibitishwa. Kwa kuwa hazijathibitishwa, siwezi kuzungumzia kiundani,” alisema Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.
 
“Nachoweza kusema ni kwamba chama chetu kina utaratibu, kinatabirika na kinaeleweka. Hakuna haja ya kuwa na papara katika hili na mimi sina hofu na hili kwa kuwa najua kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa.”
 
Alisema anajua kuwa uteuzi utafanyika miezi miwili kabla ya uchaguzi ili utakapofika mwezi Agosti chama kipeleke majina kwenye Tume ya Uchaguzi yakiwa yamechujwa kwa umakini bila ya kuwa na papara ya aina yoyote.

Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambao wote wanatajwa kuwamo kwenye mbio za urais, hawakutaka kuzungumzia suala hilo, Membe akisema yuko safarini kikazi na Sumaye akisema hajasikia habari hizo.
 
Juhudi za kumpata Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa hazikufanikiwa.

Credit: Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post