TAARIFA ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA AJABU ULIOIBUKA HUKO SIMIYU,WATU WANAONGEA OVYO NA KUANGUKA


Hali ya taharuki imewakumba wananchi katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, baada ya kuibuka ugonjwa wa ajabu uliowakumba wananchi hao ambao dalili zake ni kuongea ovyo, kuishiwa nguvu pamoja na kuumwa kichwa.

Bado haijajulikana ni aina gani ya ugonjwa kutokana na baadhi ya waathirika waliofikishwa katika vituo vya afya kupimwa na kubainika hawana ugonjwa wowote na badala yake kubaki wakiweweseka.

Mkuu wa wilaya hiyo Erasto Sima alisema kuwa ugonjwa huo ulianza usiku wa kuamkia tarehe Mei 02,2015, katika kata za Mwandoya, Mwabusalu, Lingeka, Mwakisandu, Tindabuligi, Pamoja na Lubiga.

Sima alieleza kuwa tangu kuibuka kwa ugonjwa huo idadi ya wagonjwa imezidi kuongezeka kila siku, ambapo alibainisha kuwa mpaka jana wamefikia jumla ya wagonjwa 80 kutoka katika kata hizo.

Sima aliongeza kuwa timu ya wataalamu, wahudumu wa afya, pamoja na madaktari kutoka katika hospitali ya wilaya hiyo, tayari wamewasili katika kata hizo kwa kushirikina na wataalamu wa afya waliopo ili kuongeza nguvu kutoa huduma ya kwanza.

Alisema kuwa wagonjwa mbalimbali ambao wamekuwa wakiletwa wamekuwa wakionyesha dalili na kuishiwa nguvu, kuongea maneno yasiyoeleweka, kuwapiga wenzio, kugongwa na kichwa, kutokwa na mafua, ikiwa pamoja na kukohoa kikohozi kikavu.

Alieleza kuwa ofisi ya mganga mkuu wa mkoa iliwasili baada ya kutokea kwa ugonjwa huo, ambapo sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya kupelekwa katika hospitali ya rufaa Bugando iliyoko Mkoani Mwanza kwa ajili ya vipimo ili kubaini ni aina gani ya ugonjwa.

Alisema taarifa alizozipata ambazo hana uhakika nazo kutokana na kutokudhibitishwa na wataalamu, kuwa ugonjwa huo unaambukizwa na wanyama wa porini kwa kile alichoeleza baadhi ya waathirika  wanapakana na pori tengefu la Maswa.

Hata hivyo aliongeza kuwa awali walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kabla ya kutokea ugonjwa huo kwao mifugo ikiwemo ngo’mbe ilikuwa ikishika na ugonjwa huo kwa kuweweseka hadi kupoteza uhai.

Aliongeza kuwa bado hawajatambua ugonjwa huo unaambukizwa kwa hewa, au kushikana mikoni kwa kile alichoeleza bado wanasubilia majibu ya vipimo vilivyochukuliwa katika hospitali ya rufaa bugando.

“ Bado hatujatambua dalili zake ni nini? Unaambukizwaje?.. kutokana na vipimo vilivyopelekwa vikiwa bado havijarejeshwa…lakini huduma ya kwanza inaendelea kutolewa na tumeongeza nguvu za kutoa huduma hizo” Alisema Sima.

Aliongeza kuwa ugonjwa huo unawashika watu wote wakiwemo watoto, huku akieleza kuwa afisa mifugo na misitu ametumwa katika ameneo hayo ili kuchunguza kama ugonjwa huo unasababishwa na wanyama kama ilivyoelezwa na wananchi hao.

Kuhusu ugonjwa kuhusishwa na imani za kishirikina mkuu huyo wa wilaya alikanusha habari hizo na kueleza kuwa hakuna dalili ambazo zimeoneshwa kuwa ugonjwa huo unatokana na imani za ishirikina.

Aliongeza kuwa baadhi ya wagonjwa ambao wamefika kupatiwa huduma kutokana na ugonjwa huo, walikutwa na magonjwa mengine mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa maralia ambao alisema walitibiwa na kupona hadi kuruhusiwa kwenda nyumbani.


Alipotafutwa mganga mkuu wa wilaya hiyo Majeda Kihulya alikataa kuongelea suala hilo, huku akieleza kuwa majibu ya vipimo vilivyopelekwa Bugando yatakapoletwaa na Mkuu wa wilaya husika ndiye atakayetoa katika vyombo vya habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post