RAIS WA MOCU AWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA AMANI

Rais wa serikali ya Wanafunzi wanaosoma katika chuo kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Shinyanga (MOCU) Bright Dominic Muro

Rais wa serikali ya Wanafunzi wanaosoma katika chuo kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Shinyanga (MOCU) Bright Dominic Muro amewataka watanzania kudumisha amani ya nchi ikiwemo kutowafanyia ukatili watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa kuwakata viungo vyao.

Rais huyo wa MOCU ( Moshi Cooperative University) ameyasema hayo juzi katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wanafunzi wa chuo hicho wakikabidhi msaada wa chakula na mahitaji mbalimbali muhimu kwa ajili ya watoto hao.

Muro alisema amani ya taifa siyo tu taifa kuwa huru dhidi ya vita wala mapigano bali ni watu wanaoishi katika taifa hilo kuwa na amani hivyo kuitaka jamii kwa kushirikiana na serikali kupiga vita kwa nguvu zote mauaji ya abino yanayowafanya waishi bila amani katika taifa lao.

Alisema amani kamili katika taifa ni pale watu katika jamii wanapoishi na amani bila hofu yoyote na kuongeza kuwa amani ya Tanzania imeanza kupotea kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi jambo linalosababisha nchi ionekane kukosa amani.

“Tunalaani mauaji ya albino yanayoendelea nchini,sisi kama serikali ya wanafunzi na sehemu ya jamii ya Tanzania tumeanzisha kampeni ya kupinga mauaji ya albino,hata msaada tuliokabidhi umetokana na mchango wa wanafunzi”,aliongeza Muro.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya mfuko wa kuchangia  albino katika chuo kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Shinyanga (MOCU) Neema Medard Ngaita alisema mauaji ya albino yanatokana na umaskini wa kifikra kwa baadhi ya watu kuamini kuwa viungo vya albino vinaleta utajiri na vyeo.

Ngaita alisema ni vyema sasa jamii ikabadilika na kuachana na tabia ya kuua albino na kila mtu katika jamii kuchukua jukumu la kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi.

Wakiwa katika kituo hicho wanafunzi hao walitoa misaada mbalimbali ikiwemo unga wa sembe kilo 100,maharage kilo 100,unga wa lishe kilo 40,sabuni,madaftari,mafuta ya kula na kujipaka,kalamu,nguo na viatu vyote vikiwa na thamani ya takribani shilingi 500,000/=.

Wanafunzi hao pia walishiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya usafi wa mazingira na kufua nguo za watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

Akizungumza wakati wa kupokea misaada hiyo Mwalimu wa elimu Maalum katika shule ya msingi Buhangija Sasu Nyanga kwa niaba ya mkuu wa kituo cha Buhangija mbali na kuwashukuru wanafunzi hao pia aliitaka jamii kuendelea kuwasaidia watoto wanaolelewa kituoni hapo ambao sasa wako zaidi ya 400.
 
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post