Utafiti Mpya !! NUSU YA WATANZANIA WOTE WAMEWAHI KUIBIWA MALI ZAO


Wananchi watatu kati ya kumi (30%) wamesha kukumbana na wizi ndani ya kipindi cha mwaka jana. 

Kwa ujumla, nusu ya Watanzania wote wamewahi kuibiwa.

Asilimia 84 ya wananchi wanaamini kuwa kuna uwezekano wa wao kuathiriwa na makundi ya vijana wahalifu kama Panya Road.

 Mwezi Januari 2015, Panya Road ilileta wasiwasi mkubwa jijini Dar es Salaam kwa kufanya vitendo vya uhalifu na vurugu, tukio hili lilitawala mijadala kwenye mitandao ya kijamii na kupelekea mamia ya vijana hao kukamatwa. 

Wananchi sita kati ya kumi (60%) kitaifa wamewahi kusikia kuhusu Panya Road lakini karibu wananchi tisa kati ya kumi (87%) walisema hakuna kikundi kama hicho katika maeneo yao.

Wananchi wawili kati ya kumi (18%) wameripoti kuwa walishuhudia ghasia wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Desemba 2014. 

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wake wa utafiti wenye jina la Je, tuko Salama? Maoni ya wananchi juu ya usalama na haki

Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu ya mkononi. 

Takwimu hizi zilikusanywa kwa wahojiwa 1,401 kutoka Tanzania Bara (Zanzibar haimo katika matokeo haya) mwezi Februari na Machi 2015.

Licha ya kuongezeka kwa matukio ya vurugu za kisiasa pamoja na wizi na hofu juu ya makundi ya vijana wahalifu, wananchi nane kati ya kumi (79%) walisema hawajawahi kabisa, au wamewahi mara chache kujihisi kutokuwa salama katika jamii zao na maeneo wanayoishi. 

Hata hivyo, wananchi wanaamini kuwa mfumo wa sheria haufanyi kazi ipasavyo. 

Zaidi ya nusu ya wananchi (53%) wanaamini kuwa mwananchi wa kawaida ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria akitenda kosa. 

Lakini kuadhibiwa kwa watu wenye kipato cha chini ni vigumu sana. 

Wananchi wachache (14%) wanaamini kuwa watu wenye kipato cha juu wanaweza kuadhibiwa iwapo wanavunja sheria, na wengine (21%) wanaona hili pia linawezekana kwa watumishi wa umma.

 Idadi hii imeshuka ukilinganisha na takwimu za mwaka 2013 ambapo asilimia 39 ya wananchi  walidhani kuwa watumishi wa umma watakumbana na mkono wa sheria wanapotenda makosa. 

Pamoja na haya yote, wananchi sita kati ya kumi (60%) wanaamini jeshi la polisi linawahudumia zaidi watu wenye pesa kuliko watanzania wa kipato cha chini.

Licha ya kuwa na imani kwamba polisi wanapendelea matajiri, wananchi wanne kati ya kumi (37%) waliripoti kwenda polisi wanapokumbana na uhalifu. 

Idadi hiyo hiyo (32%), wanategemea vikundi vya ulinzi vya kijamii au kamati zao za kijiji/mtaa. 

Baadhi hawaendi kutoa taarifa polisi kwa sababu ya rushwa (29%), na wengine kwasababu polisi hawatawajali (14%). 

Inaonekana kwamba matukio ya ukatili dhidi ya polisi yameongezeka.

 Wananchi wawili kati ya kumi (21%) wameyasikia matukio ya aina hii. Mwaka jana (2013) ni mwananchi mmoja tu kati ya kumi aliyeyasikia matukio kama haya. 

Kutokana na imani ndogo na jeshi la polisi kama wanavyoripoti wananchi, watu wengi wameanzisha vikundi vya usalama vya kijamii ambavyo husimamia utekelezaji wa sheria za kawaida. 

Taarifa nyingi za uhalifu na vurugu zinapelekwa huko, huku wananchi watatu kati ya kumi (29%) wakiripoti kuwahi kusikia matukio ya vitisho, watu kupigwa na vikundi hivi vya usalama.

Elvis Mushi, Meneja wa Sauti za Wananchi alisema "Wananchi wanakabiliwa na wizi, hofu ya magenge na kukosekana kwa usalama ifikapo kipindi cha uchaguzi. Pia wanahisi kwamba vyombo vya sheria vinaupendeleo. Hii ni changamoto kwa watunga serikali. " 


Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, aliongeza kwa kusema " Kwanza, wananchi wengi wanajihisi kuwa salama katika maeneo yao lakini bado wanakumbana na vitendo vya wizi, wanaogopa kuvamiwa na vikundi kama Panya Road na baadhi yao kushuhudia ghasia na vurugu za kisiasa. 

Aidha, wananchi wameshuhudia ongezeko la ukatili dhidi ya vituo vya polisi ndani ya miaka miwili iliyopita, jambo hili linapunguza imani yao na vyombo vya usalama. 

Usalama una umuhimu wa kipekee katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Rai yetu ni kwa serikali kuyazingatia maoni haya ya wananchi katika utekelezaji wa jukumu lake la kuwahakikishia wananchi usalama wa hali na mali."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post