Ikulu
imesema Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya
Mtandao ya mwaka 2015, kwa kuwa umepitia taratibu zote. Pia, Ikulu
imesisitiza kuwa sheria hiyo ni nzuri na itadhibiti matumizi mabaya ya
mtandao.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alitoa taarifa hiyo jana,
alipozungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rweyemamu alisema sheria ya Makosa ya Mtandao itasainiwa na rais muda
wowote.
“Hii
ni sheria nzuri, kwanza inadhibiti matumizi mabaya ya mitandao, wote
watakaohusishwa ama kutuma au kutumiwa vitu au picha mbaya sheria
itawabana wote, na kama umetumiwa bila idhini yako, toa taarifa polisi,
ili uwe kwenye upande salama,” alisema Rweyemamu.
Alisema madai ya wadau kwamba inanyima uhuru wa kupata taarifa, hayako sahihi kwa kuwa hiyo si sheria ya habari.
Alisema kutokuwa na sheria hiyo, si jambo jema kwa usalama wa nchi.
Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ulipitishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge, uliofanyika Dodoma hivi karibuni.
Katika
mjadala, wabunge wengi walikemea vitendo vilivyokithiri vya uhalifu wa
mtandao nchini, na kutaka sheria hiyo itakaposainiwa, itumike ipasavyo
kudhibiti.
Wabunge
wengi walisema viongozi, watu maarufu na jamii kwa ujumla, wamekuwa
waathirika wakubwa wa matumizi hayo mabaya ya mtandao, kutokana na
kutukanwa, kutishiwa kuuawa, kuzushiwa uongo na hata wakati mwingine
kutapeliwa.
Hata
hivyo, baada ya kupitishwa muswada huo, kumekuwapo na kauli za ukosoaji
kutoka kwa watu binafsi na makundi mbalimbali, wakitaka rais asisaini
hadi baadhi ya vifungu virekebishwe.
Miongoni
mwa mambo yaliyokosolewa ni pamoja na sheria kubana pia mtu anayetumiwa
vitu au picha mbaya . Wakati huo huo, Rweyemamu akizungumzia Muswada wa
Sheria ya Takwimu kuhusu maombi ya wadau ya kutaka ziangaliwe pande
zote mbili wakati wa kutiwa hatiani, kutokana na kutoa au kuandika
takwimu zisizo sahihi. Alisema maombi hayo yatazingatiwa.
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Habari, uliopelekwa pia katika mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni, Rweyemamu alisema;
“Mimi
naomba wadau wa habari wauunge mkono muswada huu, madai kuwa umepelekwa
bungeni chini ya hati ya dharura sio kosa, na pia madai kuwa
haujajadiliwa na wadau nalo sio sahihi, kwani muswada huu umejadiliwa
zaidi ya miaka 10, na mimi pia nilishiriki kwenye moja ya mkutano wa
wadau kuujadili miaka hiyo pale Morogoro.”
Aidha
alisema kuendelea kupinga muswada huo ni kusababisha kuendelea kuwa na
sheria ya zamani, jambo ambalo linafanya kukosa sheria mpya. Alisisitiza
wadau wa habari kuunga mkono .
Ugaidi
Akizungumzia
masuala ya ugaidi, Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano Ikulu alishukuru
vyombo vya habari kwa kuandika na kuripoti habari za ugaidi kwa
kuhabarisha wananchi mbinu za kujihami, iwapo tukio hilo litatokea.
Aliomba viendelee kuhabarisha umma taarifa za kujenga na kujihami dhidi ya matukio hayo, bila kuongeza chumvi na ushabiki.
“Navishukuru
vyombo vya habari vimefanya kazi yao ya kuhabarisha umma kuhusu masuala
ya ugaidi na mbinu za kujihami, ila kuna baadhi wamekuwa wakiandika
habari hizo kwa ushabiki na kuongeza chumvi, jambo ambalo siyo zuri,” alisema.
Social Plugin