Wanawake wajane ambao ni Wafugaji jamii ya Kimasai, wamejikuta
wakiangua kilio katika kituo cha Polisi Mvomero, mkoani Morogoro baada
ya kukabidhiwa idadi pungufu ya ng'ombe zilizokamatwa baada ya kuporwa
na kundi la ulinzi wa jadi la wakulima.
Walinzi hao wa jadi kutoka katika kijiji cha Dihombo, lilivamia
Kijiji cha Kambala ambacho wanaishi wafugaji hao na kupora ng'ombe 145
kwa madai kuwa wafugaji wa kijiji hicho kuwapora wakulima wenzao
pikipiki tatu na kusababisha uhalibifu wa trekta wakati wakielekea
shambani katika bonde la Mgongola na pikipiki hizo kutelekezwa porini.
Mmoja wa wanawake hao, Belitha William, alisema akiwa kijijini
Kambala akiendelea na shughuli za kuchunga mifugo yake, ghafla
alivamiwa na kundi la vijana wenye silaha za jadi maarufu kama muano na
kupora ng'ombe wake wapatazo 145 pamoja na ndama na kuondoka nao.
Alisema baada ya kuona kundi hilo la vijana yeye na familia yake na
wafugaji wengine walikimbia katika eneo hilo kwa ajili ya kusalimisha
maisha yao na ndipo kundi hilo likamua kuondoka na mifugo hiyo na kwenda
nayo katika ofisi ya kijiji cha Dihombo.
Mfugaji huyo alisema alipoifuatilia mifugo hiyo alielezwa inalindwa
na kundi la walinzi wa jadi mpaka pale wafugaji wa jamii hiyo ya
kimasai watakaporudisha pikipiki walizopora wafugaji wenzao.
Hata hivyo, alisema baadaye mifugo hiyo ilipelekwa ofisi ya Tarafa
ya Mvomero kwa ajili ya kupigwa faini mifugo hiyo kuzurura katika
mashamba huku mingine ikiwa haipo.
Kwa upande wao, wakulima walioporwa pikipiki hizo, Fabian Clement
pamoja na Francis Boniface, wakielezea tukio la kuporwa pikipiki hizo,
walisema kwa nyakati tofauti kuwa wakati wakielekea katika mashamba ya
bonde la Mgongola kwajili ya kuwapelekea chakula wenzao, waliona kundi
kubwa la wafugaji jamii ya Wamasai wakiwa na silaha za jadi pamoja na
bunduki likiwafuata ndipo walipokimbilia porini.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Mussa Malambo,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa baada ya polisi
kupata taarifa hizo walifanikiwa kwenda katika eneo hilo na kuwataka
wakulima hao kuzifikisha ng'ombe hizo katika ofisi ya Tarafa na tayari
mwenye ng'ombe hao wamekabidhiwa baada kupigwa faini.
Na Ashton Balaigwa -Nipashe
Na Ashton Balaigwa -Nipashe