Taarifa ya Polisi Vurugu za Iringa!! 18 WAKAMATWA,POLISI MMOJA YUKO HOI HOSPITALI,ALIYEFARIKI ATAJWA



Mwanamke mmoja  amefariki dunia mkoani Iringa baada ya kutokea kwa vurugu kati ya askari polisi na wananchi maeneo ya Ilula wilaya ya Kilolo  ambapo jeshi la polisi pia linawashikilia wananchi 18 wa eneo hilo kwa mahojiano zaidi.
Hayo yamesemwa leo na kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa ACP Pudensiana Protas  wakati akiongea na waandishi wa habari ambapo amemtaja aliyefariki katika vurugu kuwa ni bi  Mwaine Mtandi  (25) mkazi wa kijiji cha Dingizayo wilaya ya Kilolo  mkoani Iringa.
Amesema mwanamke huyo alikuwa akijihusisha na uuzaji wa pombe za kienyeji na alifariki papo hapo baada ya kuanguka wakati akijaribu kuwakimbia polisi waliokuwa kwenye oparesheni ya kukamata makosa mbalimbali ya jinai.
Kaimu Kamanda Protas amesema tukio hilo limetokea jana  majira ya saa nne na nusu asubuhi wakati polisi  wakiwa kwenye zoezi la kawaida la msako wa makosa mbalimbali ya jinai ikiwa ni pamoja na kuwakamata wanaojihusisha na vitendo vya uuzaji wa pombe haramu ya gongo na ufunguaji wa vilabu vya pombe za kienyeji muda wa kazi.
Amesema baada ya kutokea kwa kifo hicho wakazi wa eneo la Ilula walianza kuandamana kisha kuifunga kwa kuichoma moto barabara kuu ya Iringa-Dar es Salaam ,wakitumia tairi za magari,nyasi na karatasi hali iliyopelekea kusimama kwa shughuli za usafirishaji kwa magari kutoka mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam pamoja na Mbeya,Njombe na Ludewa.
Aidha amesema wananchi hao walivamia kituo kidogo cha polisi cha Ilula na kuvunja vioo vitano,kuchoma moto nyaraka mbalimbali pamoja na kuteketeza kwa moto magari matatu ambayo ni gari la kituo hicho,gari la mmoja wa polisi wa kituo hicho pamoja na gari moja ambalo lilikuwa limekamatwa kama kielelezo.
Kaimu Kamanda Protas ameongeza kuwa wananchi hao walitumia silaha mbalimbali za jadi ikiwa ni pamoja na mawe,rungu na mapanga hali iliyopelekea majeruhi kwa askari watano ambapo wanne walipata huduma ya kwanza na kuruhusiwa na mmoja wao bado anaendelea na matibu katika hospitali ya mkoa wa Iringa.
Amesema kufuatia vurugu hizo jeshi la polisi mkoani Iringa linawashikilia watu 18 kwa uchunguzi zaidi huku wananchi wawili wakiendelea na kupatiwa matibabu katika hospitali teule ya wilaya ya Kilolo baada ya kujeruhiwa katika vurugu hizo.
Kaimu kamanda Protas ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kwa ujumla kutojichukulia sheria mkononi pindi yanapotokea matukio mbalimbali na  kuongeza kuwa uchunguzi zaidi wa vurugu hizo unaendelea ikiwa ni pamoja na kubaini chanzo halisi cha mauaji hayo.
Hali hiyo imekuja kutokana kutofautiana kwa wakzi wa eneo hilo juu ya chanzo cha halisi cha mauaji hayo ambapo wapo waliodai kifo hicho kimetokana na marehemu kupigwa risasi,na wengine kuongeza kuwa alipigwa rungu huku baadhi yao wakidai kuwa alipigwa mtama na polisi katika harakati za kumkamata marehemu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527