Taswira eneo la mgodi wa Bulyanhulu-Kahama |
Wananchi wa
kijiji cha Namba Tisa katika kata ya Bulyankulu wilayani Kahama Mkoa wa
Shinyanga wameulalamikia mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu kwa
kutiririsha maji yenye sumu ya sayanaidi (CYANIDE) kwenye mashamba yao.
Hayo yamebainishwa
jana na Wananchi wa kijiji hicho, kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Mkuu wa
wilaya hiyo Benson Mpesya ambapo mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili
athari za sumu hiyo.
Wananchi hao
walisema maji hayo ya sumu yameathiri mazao yao, waliyokuwa wamelima kwa ajili
ya chakula na biashara, jambo ambalo walisema linawarudisha nyuma kimaendeleo.
“Ndugu Mkuu wa
wilaya sisi kama wananchi wa kijiji hiki tulikuwa tumelima mpunga, nyanya, na
tulikuwa tumepanda miti ya matunda lakini vyote vimekauka kutokana na sumu
inayotoka mgodini ,tunaomba utusaidie kwa hilo,”walisema wananchi hao.
Walisema kutokana na sumu hiyo kuzagaa kila mahala ,wamekuwa wakipata shida kubwa sehemu ya kunyweshea mifugo yao, hivyo wameiomba serikali iingilie kati suala hilo.
“Jambo hili
limetuathiri sana wafugaji, kwani hatuna sehemu ya kunyweshea mifugo yetu, hali
inayotulazimu tuuze mifugo yetu kwa hasara kwa wachinjaji wa nyama, ili mifugo
hiyo isife kwa kukosa maji”,waliongeza wananchi hao.
Baada ya kupokea
malalamiko hayo Mpesya, aliwaomba wananchi hao wawe watulivu wakati serikali
inalishughulikia suala hilo kwa muda mfupi na kuwataka wananchi wasitumie maji
hayo kwa shughuli yeyote.
“Kwanza
nimejionea mwenyewe jinsi sumu ilivyozagaa na mazao yenu yalivyokauka na
kuharibika poleni sana kwa hilo, lakini nalishughulikia ndani ya muda mfupi
suala hili litaisha, na malalamiko yenu nimeyasikia na kuyapokea ila naombeni
msitumie maji haya kwa shughuli yeyote iwe kunywa, kuoga wala kupikia ni hatari
sana”,alisema Mpesya.
Kwa upande wake
Msemaji wa Mgodi huo Abdallah Msika, alikiri kuwepo kwa sumu hiyo kuzagaa
kwenye mashamba ya wananchi hao, ambapo alisema kuzagaa kwa sumu hiyo
kulisababishwa na mvua kubwa kunyesha hali iliyopekea bwawa la mgodi huo kujaa
maji na kutiririsha mpaka kwenye mashamba.
Hata hivyo Afya
za wakazi wa kijiji hicho, ziko hatarini kutokana na maji hayo ya sumu ya
Sayanaidi (CYANIDE), ambapo watu 15 wamebabuliwa ngozi zao na sumu hiyo hatali
kabisa.
Na Valence
Robert-Malunde1 blog Kahama
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba +255 688 405 951