Sherehe za Kutahiriwa zageuka msiba!! KIJANA AUAWA AKIGOMBANIA MSICHANA HUKO MARA



Sherehe za kutahiriwa zimegeuka kuwa msiba, baada ya vijana kumshambulia kwa rungu na kumuua mwenzao wakati wanaserebuka kusherehekea kutoka jandoni, zilizokuwa zinafanyika Bunda mkoani Mara.

 Kufuatia mauaji hayo, watu  watano wakiwamo watoto watatu  wanashikiliwa na polisi  wilayani  Bunda, kwa tuhuma za kumuua kijana mwenzao kwenye ugomvi wa kugombania msichana uliotokea kwenye sherehe hizo za  tohara.

Kamanda wa Polisi  wa Mkoa , Phillipo Kalangi, alisema mauaji hayo yalifanywa  usiku wa kuamkia juzi katika kitongoji cha Bunda Stoo, mjini Bunda.

Kalangi alimtaja  aliyeuawa kwa kupigwa na rungu kichwani kuwa ni Mandela James (25) mkazi wa mtaa wa Saranga mjini Bunda.

Kwa mujibu wa Kalangi wanaoshikiliwa ni  watoto wawili wenye miaka 16  na  mmoja mwenye miaka 17 ambao majina yanahifadhiwa kutokana na umri wao kuwa mdogo , Ghati Robhi (26), Justun Robhi (19)  ambao wote ni wakazi wa mjini Bunda. Uchunguzi unaendelea kabla ya kuwafikisha mahakamani.

 Alisema  wakati vijana hao wakiendelea kucheza muziki,  wawili kati yao waligombania msichana ndipo mwenzao mmoja akachukua rungu na kumpiga James kichwani na  kufa papo hapo.

Kwa mujibu wa mila za Wakurya, vijana huenda porini kwa wiki mbili kutahiriwa na wazee wao na baada ya kupona hurudi nyumbani ambapo sherehe kubwa hufanyika ikihusisha kula nyama  za ng'ombe , mbuzi na pombe pamoja na kucheza ngoma mbalimbali likiwamo ritungu.

 Na Ahmed Makongo-Mara

Bonyeza hapa Tukupe habari zote mara moja zikitoka "HABARI" VITUKO "MAPENZI"MAGAZETI,UDAKU>
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba  +255 688 405 951

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527