Sakata la wizi wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta escrow zaidi ya bil 300 limeendelea kukitesa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Geita baada ya wananchi kuamua kususia mikutano ya chama hicho na kusababisha wagombea wake kunadi sera zao mbele ya watoto.
Katika mkutano wake uliofanyika juzi kwenye uwanja wa soko la mtaa wa mkoani mjini Geita,uliokuwa uhutubiwe na mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Geita Vicky Kamata kabla ya kuingia mitini,baadhi ya viongozi wa chama hicho walijikuta wakiwa peke yao na wanachama wao wachache wenye sare za chama hicho huku wananchi wakisusia mkutano huo na kuendelea na mambo yao.
Wakizungumza na mwandishi wa Malunde1 blog Valence Robert ,kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa mtaa wa mkoani waliokutwa wakifanya shughuli zao bila kusogea katika mkutano huo walidai kuwa hawaoni sababu ya kuwasikiliza wanaCCM kwa kuwa Rais Kikwete haoneshi nia ya dhati kuwawajibisha watuhumiwa wa Escrow.
''Ndugu yangu kwa hali ilivyo hapa nchini tumeamua hata tusihudhurie mikutano yao kabisa hawa watu ili wajifunze,yaani safari hii ni bora tuchague jiwe kutoka chama kingine na si chama cha mapinduzi,tumechoka kaka’’alisema Mabula Kaloli mkazi wa mtaa wa mkoani aliyekutwa akicheza karata na wenzake umbali wa zaidi ya mita 300 kutoka eneo la mkutano.
Mwingine ni Mayala Kubingwa aliyedai kuwa,wakati nchi inatimiza miaka 53 ya uhuru wa kutokuwa na uhuru hakuna mtanzania hususani wa Geita anayeweza kusherehekea miaka hiyo,wakati hakuna huduma za kijamii na kudai kuwa iwapo chama hicho kingekuwa na nia ya kuwakomboa watanzania kingenyonga mafisadi wote wa Escrow.
Hata hivyo,katika hali isiyokuwa ya kawaida,siku moja kabla ya mkutano huo pamoja na gari la matangazo kuwatangazia wananchi kwamba mkutano huo utahutubiwa na Mbunge wa viti maalumu mkoa wa Geita Vicky Kamata ambaye angemnadi mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa mtaa wa mkoani, hali ilikuwa tofauti baada ya mbunge huyo kuingia mitini baada ya kupigiwa simu na kuelezwa kuwa hakuna wananchi wengi kwenye mkutano huo na kuja kwake eneo hilo kungemletea fedheha kutokana na ukubwa wa jina lake.
Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Kamata ili kujua sababu za kutokuhudhuria mkutano wake simu yake ya kiganjani iliita pasipo kupokelewa na baadaye ilizimwa.
Hata hivyo vyanzo vyetu kutoka ndani ya chama hicho vilidai kuwa chanzo cha mbunge huyo kukacha mkutano huo ni kuhofia zomeazomea ambayo imekuwa ikikizonga chama hicho pamnoaj na uchache wa wananchi wanbaohudhuklia mikutano yao.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita
Mtandao Huu Unakujali,Ni Wako!! Tunataka Tukutumie Habari zetu Zote Mara Tu Tunapozipandisha Mtandaoni.Kujiunga nasi Bonyeza Hapa Sasa Hivi ><<VITUKO>>,"MAPENZI",<<HABARI MSETO>>MAGAZETI
Mtandao Huu Unakujali,Ni Wako!! Tunataka Tukutumie Habari zetu Zote Mara Tu Tunapozipandisha Mtandaoni.Kujiunga nasi Bonyeza Hapa Sasa Hivi ><<VITUKO>>,"MAPENZI",<<HABARI MSETO>>MAGAZETI


Social Plugin