CCM WAIPIGIA SALUTI UKAWA,UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA TANZANIA



Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakiri kuporomoka zaidi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongozi uliofanyika Jumapili, tathmini inaonyesha kuwa harakati za vyama vya upinzani zimezidi kufanikiwa kwa kuendelea kumega ngome ya chama tawala katika maeneo mengi nchini.


Ingawa CCM iliingia kwenye uchaguzi huu ikiwa na faida ya kupita bila kupingwa katika vijiji 2,708, mitaa 644 na vitongoji 26,300, mafanikio ya upinzani yanaonyesha kuwa mikakati yao kama vile Movement For Change (M4C), Vua Gamba Vaa Gwanda; Delete CCM na mkachamchaka kuelekea mwaka 2015 (V4C), imekuwa na faida kwao kulingana na matokeo ambayo yamekwisha kutangazwa tangu Jumapili hadi jana.

Mabadiliko ya kisiasa kwa ngome ya CCM kuzidi kumomonyolewa na upinzani chini ya mwavuli wa Umoja wa Kutetea Katiba (Ukawa), yalithibitishwa jana na chama hicho kuwa kimeporomoka kwa asilimia 12 katika matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliyofanyika Jumapili iliyopita.

Chama hicho kimesema kimeporomoka kutoka asilimia 96 mwaka 2009 hadi kufikia asilimia 84 mwaka huu.Aidha, kimesema kushuka kwa matokeo hayo hakiyahusishi na sakata la uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow, yametokana na makosa yaliyofanyika ndani ya chama wakati wa uteuzi wa wagombea wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema asilimia 16 ya viti walivyopata wapinzani bado ni ndogo ikilinganishwa na miaka 22 tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Alisema, matokeo hayo ni ya nchi nzima katika maeneo yote ambayo tayari matokeo yameshatangazwa na Tamisemi.“Haya matokeo hatuwezi kusema tumepoteza sana kwani tulitarajia kuwa na matokeo yanayotokana na mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini cha kusikitisha pamoja na juhudi za kuungana kwa wapinzani na kuunda Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) wameweza kupata asilimia 16 tu, wakati ni miaka 22 sasa tangu kuanzishwa kwa mfumo huu, hii ni wazi kuwa CCM bado inapendwa na kukubalika,” alisema Nape.

Akielezea sababu za kuporomoka kwa chama chake katika uchaguzi huo, Nape alisema ni kutokana na migongano ya ndani ya chama ambayo ilisababisha wajumbe kuteua watu wasiofaa na wasiokubalika kwa wananchi.

Alisema maamuzi waliyoyafanya wananchi ya kuchagua upinzani ni mazuri kwani wameonyesha demokrasia ya kweli ambayo CCM waliona ni nzuri ndio maana wakaingia kwenye mfumo wa vyama vingi.




“Nawapongeza wananchi kufanya maamuzi ya kile ambacho wamekiamini, hii ndiyo demokrasia, tulitarajia kuwa na ushindani, hivyo ni vyema wenzetu nao wakawa na sehemu ya ‘kupumulia’  siyo tuwe CCM tu. Nawashauri watumie vyema dhamana waliyopewa na wananchi na CCM bado tutaendelea kuwatumikia wote vyema,” alisema Nape.

Akifafanua kuhusu sakata la fedha za Escrow, Nape alisema katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambako Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alikuwa akifanya ziara hakuwahi kulalamikiwa kuhusiana na sakata hilo zaidi wananchi walitaka kutatuliwa matatizo yao yakiwamo maji na korosho.

“Tunaendelea kufanya tathmini ili kufahamu sababu za kushuka kwa matokeo haya, ila hatuwezi kuyahusisha na sakata hili, wananchi wanachotaka ni kutatuliwa matatizo yao si vinginevyo, na maamuzi ya wananchi ni ya kidemokrasia, japo wengine walichagua upinzani kwa hasira,” alisema Nape.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwakani, Nape alisema matokeo hayo hayawezi kuwaathiri kwa sababu huu ni uchaguzi mdogo ambao ni kama kura za maoni na watu wengi hawakupata fursa za kujiandikisha katika uchaguzi huo.

Alisema zoezi la uandikishaji lilikuwa na muda mfupi, hivyo watu wengi hawakujitokeza, na kwamba anaamini bado CCM kina nafasi kubwa ya kuendelea kushinda.
Alisema pia CCM hakikufanya kampeni za kutosha katika maeneo mengi kama ambavyo upinzani walifanya kampeni za jumla na kwamba uchaguzi wa mwakani bado wana nafasi nzuri zaidi.
Alisema pia yapo makosa ambayo yalishindwa kupatiwa ufumbuzi kabla ya uchaguzi kama rushwa na upendeleo ambayo yalifanya wagombea wenye sifa kuachwa na kuteuliwa wagombea wasio na sifa, hali iliyosababisha CCM kupoteza viti.

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kupata wagombea kama ndio uliowakosesha viti, Nape alisema kila mwaka wa uchaguzi taratibu zinabadilika na kwamba hakuna utaratibu ambao unaweza kubadili matokeo ya uchaguzi.

KASORO ZA UCHAGUZI
Aidha, Nape alisema anasikitishwa na changamoto zilizojitokeza katika zoezi la uchaguzi huo na kuitaka serikali ichukue hatua ya kuwawajibisha wale wote waliohusika katika uzembe huo.
Alisema ni jambo la kusikitisha kusikia serikali inasema inachunguza uzembe uliofanyika wakati inafahamika wazi kuwa uzembe huo ulianzia wapi.

“Inasikitisha kuona zoezi limeharibika, majina ya wagombea wamechanganywa tena hapa jijini Dar es Salaam. Watu waliohusika kupeleka fomu zilizoharibika kwenye vituo vya kupigia kura wanafahamika, wachukuliwe hatua haraka, wakamatwe watiwe ndani hakuna namna ya kuacha kuwawajibisha wakati ni uzembe wa hali ya juu,” alisema Nape.

Alifafanua kuwa serikali inapaswa kuangalia zoezi lilianza kuharibikia wapi na kuwahoji wahusika ili kufahamu nani alisababisha tatizo hilo na hatua dhidi yao zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

NANI KAPATA, NANI KAKOSA?

Tathmini ya uchaguzi huo imeonyesha kwamba vyama vyote kwa maana chama tawala na vyama vinavyounda Ukawa hususani Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vilijiandaa kwa muda mrefu.
Vyama hivyo vilifanya kampeni na operesheni na kuibua hamasa kubwa kwa wananchi kushiriki uchaguzi huo.

Ingawa CCM kimepata ushindi wa asilimia 84, lakini kikiwa kimeporomoka kwa asilimia 12 kulinganisha na asilimia 96 za mwaka 2009, operesheni za kujijenga zilizofanywa na vyama vya upinzani zimevisaidia zaidi kwa kuwa vyama hivyo vimepata ushindi hadi vijijini ambako ilikuwa ngome kubwa ya CCM.

VUGUVUGU LA MABADILIKO (M4C)
Mkakati wa M4C chini ya Chadema, ulizinduliwa mwaka juzi na Januari mwaka jana, chama hicho kiunda kanda 10 nchini na kuchagua viongozi kuanzia ngazi ya misingi, matawi, majimbo, wilaya, mkoa na taifa kwa lengo la kukipeleka chama hicho kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini.

Ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, Chadema ilitenga asilimia 40 ya fedha yake ya ruzuku kupeleka kwenye kanda hizo na pia ilinunua pikipiki 126 zilizokuwa na nembo ya M4C kwa ajili ya kufanikisha operesheni hiyo ambayo iliongozwa na falsafa yake ya ‘nguvu ya umma.’

Kadhalika, Baraza Kuu liliridhia kuandaliwa kwa mwongozo kuhusu utaratibu wa kutangaza kusudio la kugombea nafasi za uongozi kwenye chama na katika chaguzi za kiserikali kuanzia ngazi za kitongoji, kijiji/mtaa, udiwani, ubunge na urais.

OPERESHENI DELETE CCM 2014 

Operesheni hii ilizinduliwa na Chadema mapema mwezi uliopita ambayo iliendeshwa na viongozi waandamizi wa chama hicho akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Lengo la operesheni hiyo ilikuwa kuhamasisha wananchi kujiandikisha ili waweze kupigakura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kujiandaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Operesheni hiyo ilikwenda zaidi vijijini na viongozi wa Chadema walikuwa wakieleza mambo mbalimbali ya kitaifa ikiwamo Katiba pendekezwa, Mkutano wa Bunge na uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

VUA GAMBA, VAA GWANDA
Chadema pia ilifanya operesheni maalumu iliyojulikana kama “vua gamba vaa gwanda” iliyolenga kuhamasisha wananchi hususan wanachama wa CCM, kujiunga na chama hicho.

Katika uzinduzi huo ambao ulifanyika katika viwanja vya NMC mkoani Arusha, aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM mkoani humo, James Millya, alipokelewa rasmi na kukabidhiwa kadi ya Chadema.

CUF NA V4C
Kwa upande wake, Chama Cha Wananchi (CUF), mapema mwaka huu ilizindua operesheni ya mkachamchaka kuelekea mwaka 2015 (V4C), wakilenga kuingia kila kata na wilaya mbalimbali wakihamasisha wananchi kukiunga mkono chama hicho.

Operesheni hiyo ilizinduliwa mkoani Morogoro na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye alisema viongozi waandamizi wa CUF akiwamo Mwenyekiti wake, Prof. Ibrahim Lipumba, aliyeiongoza.

CCM NA VUA GAMBA
Mwaka 2011 CCM ilianzisha operesheni ‘Vua Gamba’ ikilenga kujenga taswira ya chama hicho mbele ya jamii na kuwataka makada wake waliokuwa wakituhumiwa kuhusika kwenye kashfa mbalimbali za ufisadi wajiengue wenyewe kwenye chama ndani ya siku 90.

Operesheni hiyo ambayo iliongozwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Chiligati, ilikuwa ikiwataja baadhi ya makada waandamizi ndani ya chama hicho.

Operesheni hiyo ilikwenda mbali zaidi na viongozi hao wa CCM walilenga kuwawajibisha hadi viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali wakiwataka kwamba ambao wanafahamu kuwa siyo wasafi kuanza kuondoka wenyewe kabla hawajaondolewa kwa kudhalilishwa.

Operesheni hiyo ilianza baada ya Sekretarieti ya CCM kuundwa upya baada ya kuvunjwa kukamilisha falsafa ya Mwenyekiti wake ya kujivua gamba. Hata hivyo, operesheni hiyo haikufanikiwa kwa kuwa makada waliokuwa wakitajwa hawakujiengua ndani ya chama na hawajachukuliwa hatua yoyote hadi sasa.

ZIARA ZA KUKAGUA ILANI
Mbali ya 'Vua Gamba' kwa muda mrefu sasa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Nape, wamekuwa wakifanya ziara za kukijenga chama hicho ambazo zimefanyika takribani mikoa yote Tanzania Bara.

Katika ziara hizo, viongozi hao wa CCM waliwahi kuingia kwenye mgogoro na baadhi ya mawaziri waliowaita mzigo na kupendekeza kwa Rais kwamba watimuliwe.

Baadhi ya mawaziri waliotajwa ni wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, wakielezwa kuwa wameshindwa kuwatumikia wananchi.

Mawaziri hao hawakufukuzwa na wangali kwenye nafasi zao na wengine wamehamishiwa kwenye wizara nyeti zaidi.

KINANA ALALAMIKA WATENDAJI
Kinana amekuwa akisikiliza kero za wananchi na kuzitolea ufafanuzi na mara kadhaa akilalamikia utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa serikali.

Kinana pia amekuwa akishiriki ujenzi wa miradi ya maendeleo vijijini na kuzindua kadhaa, huku akikagua Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015; na kutoa maelekezo pale ambako utekelezaji umekuwa hafifu lengo likiwa ni kukijenga chama hicho.

CHANZO: NIPASHE
Mtandao Huu Unakujali,Ni Wako!! Tunataka Tukutumie Habari zetu Zote Mara Tu Tunapozipandisha Mtandaoni.Kujiunga nasi Bonyeza Hapa Sasa Hivi ><<VITUKO>>,"MAPENZI",<<HABARI MSETO>>MAGAZETI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527