SAKATA LA ESCROW,WABUNGE HUKU,WENGINE KULE


 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jana alipangua hoja zilizotolewa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ufisadi uliofanyika katika Akaunti ya Tegeta Escrow na kuacha wananchi njia panda kwa kutokuelewa nani anasema ukweli kati yake na kamati hiyo, inayoongozwa na Zitto Kabwe.
Juzi, kamati hiyo ya Zitto iliwasilisha ripoti yake kuwa imethibitisha kuwa Profesa Muhongo amekuwa mara kwa mara akilipotosha Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba ndani ya fedha hizo hakukuwa na fedha za umma.
Kamati hiyo ilieleza kuwa imebaini kuwa Profesa Muhongo ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Singh Sethi na James Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine hilo ndilo lilikuwa sababu ya upotoshaji.
Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu hoja hiyo, Profesa Muhongo alianza kupangua hoja moja baada ya nyingine ingawa katika mjadala wa baadaye, zilihojiwa na wachangiaji wengine waliohoji uhalali wa vielelezo alivyotoa.
Kutaifisha mitambo
Jana, alieleza kuwa pendekezo la Kamati ya PAC kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe si sawa kwa kuwa kulingana na mkataba wa PPA kati ya Tanesco na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha mtambo huo ni kukiuka makubaliano katika mkataba wa PPA wa Mei 26, 1995.
“Ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara za kimataifa. Aidha, utaifishaji wa miradi ya uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza wawekezaji.”
Gharama za uwekezaji
Kuhusu taarifa ya kamati ya PAC kwamba mwaka 2004 Tanesco ilifungua shauri katika Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kiuwekezaji (ICSID 2) kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya gharama za uwekezaji, Profesa Muhongo alisema suala hilo si kweli.
Alifafanua kuwa Tanesco haijawahi kufungua shauri lolote ICSID ya London au Mahakama yoyote dhidi ya Benki ya Standard Charterd kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama inavyoelezwa na PAC.
“Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa Oktoba 31, 2010 na Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika shauri hilo la ICSID 2 ni SCBHK na Tanesco na wala siyo Tanesco na IPTL.”
Alisema Februari 12, ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana na shauri la SCBHK na Tanesco na kuwashauri wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo kutokuwa na mkataba wa kibiashara baina yao.
“Vilevile, kupitia shauri la madai Na. 60/2014, lililofunguliwa na IPTL katika Mahakama Kuu ya Tanzania Aprili 4, ilizuia utekelezaji wa maelekezo hayo,” alisema.
Uwekezaji wa Sh50,000
Profesa Muhongo alisema kuhusu madai ya PAC kuwa mtaji wa uwekezaji katika mtambo wa IPTL ni Sh50,000 na kwamba huo ndiyo ungetumika kukokotoa gharama za uwekezaji ili kulipa tozo ndogo kuliko ilivyo sasa, maelezo hayo siyo sahihi.
Alisema ukweli ni kwamba kutokana na uamuzi ya ICSID 1 ya Julai 12, 2001, gharama za ujenzi wa mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.2 milioni kama ilivyoelezwa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Profesa Muhongo alisema katika taarifa hiyo, pia imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni na mtaji utakuwa 70:30 ikiwa na maana kwamba, deni ni Dola za Marekani 89.04 milioni na mtaji ni Dola za Marekani 38.16 milioni na kwamba uamuzi huo haujabadilishwa na Mahakama yoyote au mtu yeyote.
“Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokewa kutoka mabenki ya ushirika ya Malaysia kama mkopo ni Dola za Marekani 85.86 milioni ambazo kati ya Dola za Marekani 105 milioni zilizokuwa zimeidhinishwa,” alisema na kuongeza:
“Swali la kujiuliza je, mtambo huo ulikamilikaje kwa gharama ya Dola za Marekani 85.86 milioni, huku gharama halisi ya ujenzi wa mtambo wa Tegeta ikawa Dola za Marekani 127.2 milioni?
Alisema ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi ya Dola za Marekani 38.16 milioni ambazo pia zimetumika kwenye uwekezaji na kwamba Kamati ya PAC haikuonyesha fedha hizo kuwa sehemu ya uwekezaji.
PAP na umiliki wa hisa saba
Profesa Muhongo alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa za Brela za Desemba 31, 2013, uhamishaji wa hisa saba za Mechmar katika IPTL kwenda PAP ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni mmiliki wa asilimia 70 za IPTL.
Alisema Kamati ya PAC imeeleza kuwa PAP siyo mmiliki halali wa hisa saba za Mechmar katika IPTL lakini kamati imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya Mechmer na Piper Link zilipokewa na Harbinder Singh Sethi ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP.
“Kwa uthibitisho huo, kamati inakubali kuwa hisa za Mechmer katika IPTL zinamilikiwa na PAP,” alisema Profesa Muhongo.
Akana kuwa dalali
Profesa Muhongo alisema taarifa ya Kamati ya PAC kwamba yeye ndiye aliyekuwa dalali mkuu aliyewakutanisha Harbinder Sethi na James Rugemalira siyo sahihi kuwa tangu Novemba 9, 2011, Rita iliitisha mkutano na kuwakutanisha wadau wote wa IPTL wakati yeye alikuwa hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
“Mimi kama ni dalali, udalali wangu ni kupeleka umeme vijijini. Mimi kama ni dalali udalali wangu ni kusaidia wachimbaji wadogo wa madini na kupeleka Watanzania kusoma masters (shahada ya pili) duniani kote.”
Serikali kutokuchukua tahadhari
Waziri alisema Kamati ya PAC, imeeleza kuwa Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya madai mengine yanayoweza kujitokeza kabla ya kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya escrow kitu ambacho alidai si kweli.
Profesa Muhongo alisema kinga iliyochukuliwa inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia athari yoyote ambayo ingeweza kutokea baadaye kutokana na kutolewa kwa fedha katika akaunti ya escrow.
“Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali haikuchukua tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.”
Madai ya Sh321 bilioni
Profesa Muhongo alisema hoja ya PAC kwamba imejiridhisha kuwa madai ya Tanesco ya Sh321 bilioni yana uhalali japo usahihi wake utapatikana baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na Tanesco na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha Capacity Charge haina nguvu.
“Madai ya kwamba Tanesco inaidai IPTL Sh321 bilioni msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL ni Dola za Marekani 100, sawa na Sh50,000 kwa wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola za Marekani 38.16 milioni ziliwekezwa kwenye mradi wa Tegeta,” alisema.
Profesa Muhongo alisema Bodi ya Tanesco imekana kuyatambua madai hayo ya Sh321 bilioni... “Kimsingi hata vitabu vya hesabu vya Tanesco ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG, havionyeshi kuwapo kwa deni hilo.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527