Hatari Sana!! MWANDISHI WA HABARI APIGWA NA AFISA USALAMA WA TAIFA,ANUSURIKA KUPIGWA RISASI


MWANDISHI wa habari kampuni ya Businesstimes Limited, Kassian Nyandindi anayeandikia gazeti la Majira wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ameshushiwa kipigo na kutishiwa kuuawa kwa silaha na Afisa usalama wa taifa (DSO) wa wilaya hiyo (Jina tunalo) katika hoteli ya Gold farm ya Mbinga mjini.

Habari zilizopatikana jana mjini Mbinga, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 22 mwaka huu, majira ya saa 5 usiku kwenye hoteli hiyo wakati mwandishi huyo alipokuwa anaaga kurudi nyumbani kwake.

Taarifa zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa, Nyandindi ambaye alikuwa kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Sixtus Mapunda, alishushiwa kipigo na kigogo huyo wa usalama wa taifa ambapo baadhi ya wajumbe wa UVCCM wakiwemo maafisa wa umoja huo toka makao makuu ya chama hicho, walishuhudia tukio hilo.

Aidha wajumbe hao walipoona hali inazidi kuwa mbaya, walishitushwa na kufikia hatua ya kwenda karibu na tukio hilo na kuingilia kati ili kuweza kumnusuru mwandishi huyo asiweze kudhurika, licha ya kuwa wakati huo tayari alikuwa anapigwa mateke na ngumi huku kigogo huyo akiporomosha lugha chafu akimtukana mwandishi huyo.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida inadaiwa kwamba afisa usalama huyo wa taifa, baada ya kuona mwandishi Nyandindi, amebebwa kuingizwa kwenye gari ili apelekwe nyumbani kwake ghafla afisa huyo alitoka kwenye eneo la tukio na kwenda kuchukua silaha aina ya bastola, aliyokuwa ameihifadhi kwenye gari lake ambalo alikuwa ameliegesha  nje ya hoteli hiyo.

Habari zaidi za tukio hilo zilifafanua kuwa wakati silaha hiyo akiwa ameishika mkononi tayari kwa kutaka kumfyatulia risasi mwandishi wa habari, baadhi ya wajumbe wa UVCCM waliokuwepo kwenye eneo hilo la tukio walimdhibiti afisa usalama huyo na kufanikiwa kumnyang’anya silaha hiyo, ambayo baadae ilidondoka chini na kuokotwa na mmoja wa viongozi hao wa chama kisha walimuuliza kwa nini unataka kufanya mauaji kwa mwandishi wa habari huyu ambapo alishindwa kuwa na majibu zaidi aliendelea kufoka kwa hasira huku akiporomosha matusi.

Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma, Benedict Ngwenya alisema kuwa kitendo alichokifanya DSO huyo sio cha kiungwana kwa kuwa wameshindwa kuelewa sababu iliyomfanya kutumia nguvu kubwa kutaka kupoteza maisha ya mwandishi huyo, ambaye alitumia ustaarabu kuaga kwamba anaondoka anarudi nyumbani, lakini ghafla bila sababu yoyote ya msingi alijikuta akivamiwa na kigogo huyo.

Vilevile mjumbe wa baraza la umoja huo wa vijana taifa mkoani humo, Khalfan Kigwenembe alithibitisha kuwa yeye ndiye aliyeiokota silaha hiyo, na baadae alilazimika kumrudishia baada ya kuona hasira za afisa usalama huyo zimepungua na mwandishi huyo tayari alikuwa amepelekwa nyumbani kwake.

Kwa upande wake mwandishi wa habari Nyandindi, alipohojiwa na gazeti hili kuhusinana na tukio hilo alithibitisha kuwa juzi majira ya usiku mara baada ya kuwasili katika hoteli ya Gold Farm wakitokea kwenye ziara ya Katibu mkuu wa UVCCM Sixtus Mapunda, ndipo alikumbwa na tukio hilo.

Nyandindi alifafanua kuwa baada ya kupigwa na kigogo huyo Novemba 23 mwaka huu majira ya asubuhi, alikwenda kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga ambako alifanikiwa kufungua jalada la kesi yenye namba MBI/IR/1978/2014 na kupewa fomu ya matibabu (PF 3) ambayo anaendelea kupatiwa matibabu.

Alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na sakata hilo, afisa usalama huyo wa taifa wa wilaya ya Mbinga, alikuwa akiongea kwa jazba na kusema mnauhakika na tukio hilo……………. na baadae alikata simu.

Naye Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amekiri kutokea kwa tukio hilo ambalo amedai kuwa tayari limeanza kufanyiwa kazi.

Hata hivyo Katibu wa Chama Cha Waandishi wa habari mkoani Ruvuma (RPC) Andrew Chatwanga alisema, taarifa za kupigwa mwandishi wa habari Nyandindi amezipokea na kwamba tayari ameitisha kamati ya utendaji ya chama hicho kwa lengo la kutaka kutoa tamko dhidi ya afisa usalama huyo ambaye alimshambulia mwandishi huyo kwa kumtishia kutaka kumuua kwa silaha.

Na Gideon Mwakanosya-Mbinga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527