Maskini!! MBUNGE HUYU WA CCM AZOMEWA NA WANANCHI MBELE YA BOSI WAKE,WADAI HANA LOLOTE

Mbunge wa Jimbo la Korongwe Mjini, Yusuph Nassir
Mbunge wa Jimbo la Korongwe Mjini, Yusuph Nassir, jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wananchi wake wakidai kuwa hatembelei katika jimbo lake.
Zomea hiyo ilifuatia baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kuwataka wananchi waulize maswali kwenye mkutano wa hadhara ili viongozi wake wayajibu.
Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na wananchi hao, mbunge huyo aliambulia miguno na maneno ya kebehi.

 "Hajui huyo..., hatembelei wananchi wake."
Hali hiyo ilimlazimu Kinana, kumuamuru Diwani wa kata hiyo, Robart Bago, kuanza kujibu baadhi ya kero zilizotolewa.
Hata hivyo, diwani huyo alijikuta katika wakati mgumu baada ya kushindwa kujibu maswali yaliyoulizwa na kuanza kuelezea historia mbalimbali hali iliyowafanya wananchi walipuke kumzomea.
Kitendo hicho kilimfanya diwani huyo atumie muda mwingi kuwalazimisha wananchi wamsikilize bila mafanikio.
Kinana aliamua kumuokoa diwani huyo kwa kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Mrisho Gambo, kujibu malalamiko hayo.
Kitendo cha Gambo kusimama na kuanza kujibu, wananchi walilipuka kwa shangwe baada ya kuridhishwa na majibu yake.
Awali wananchi hao, walalamikia kitendo cha halmashauri kutumia eneo la wananchi kupumzikia katika kituo cha mabasi na kukifanya eneo la kupaki magari yao.
Akijibu swali hilo Gambo alisema awali wananchi walimpatia malalamiko ya ukosefu wa choo katika kituo hicho na kwamba sasa kipo na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo ndani ya wiki moja na kituo hicho kitarudi kwa wananchi.
Aidha Gambo, aliwataka wananchi hao kuendelea kuwasiliana naye juu ya mambo au matatizo yanayotokea juu yao ili kuyapatia ufumbuzi.
Aidha, alisema pamoja na hatua alizochukua dhidi ya viongozi na wananchi wanaokiuka sheria na kanuni za nchi ni pamoja na daktari wa Hospitali ya Maguga ambaye alikuwa akiuza vifaa vya tiba.
Alisema alifuatilia suala hilo na kubaini ukweli  hivyo daktari huyo alikamatwa na kukabidhiwa kwa Takukuru na hadi sasa kesi hiyo inaendelea.
Pia aliahidi kusimamia suala la walimu kuwafukuza wanafunzi waliokosa michango mbalimbali ya shule na kwamba mzazi ambaye mtoto wake atarudishwa aripoti ofisini kwake.
Aidha, wananchi hao walipoulizwa sababu za kumzomea mbunge huyo walisema ni kwa sababu hana msaada kwao.
“Huyu mbunge hana msaada kwetu, Mkuu wa Wilaya, ndiyo amekuwa akisumbuka na sisi kwa kila tatizo tunalomueleza, kukitokea tatizo humkosi mkuu wa wilaya lakini mbunge hata kutujulia hali tu hakuna,” alisema Zaina. 

NA MARY GEOFREY-NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527