TAARIFA KAMILI KUHUSU AJALI YA BASI LA MORO BEST JANA MKOANI DODOMA

Watu 11 kati ya 17 waliofariki dunia papohapo katika ajali eneo la Pandambili wilayani Kongwa, Dodoma wametambuliwa na wanne kati yao tayari wamechukuliwa na ndugu zao.
Ajali iliyosababisha watu 56 kujeruhiwa vibaya. iliyahusisha magari mawili ambayo ni basi aina ya Scania mali ya Kampuni ya Morobest lililokuwa likitokea Mpwapwa kwenda Dar es Salaam, ambalo liligongana na uso kwa uso na lori lenye tela, lililokuwa limepakia shehena ya mabomba.
Ajali hiyo ambayo ilisababisha vifo vya madereva wa magari hayo, ilitokea meta chache kutoka mahali ilikotokea ajali iliyosababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma David Misime aliielezea tukio hilo lilitokea saa 2 asubuhi kuwa miongoni mwa ajali mbaya ambazo zimetokea mkoani humo katika siku za karibuni.
“Ni watu 17 ambao wamekufa hapa hapa, kati ya hao 12 ni wanaume na wanawake ni watano, majeruhi ni 56, kati yao tisa wana hali mbaya zaidi,” alisema Misime.
Hadi jana jioni maiti za watu kumi na moja walikuwa wametambuliwa na wanne kati yao walichukuliwa na ndugu zao.
Waliotambuliwa ni Gabriel Lemanya (Dereva wa lori) ambaye ni Mkazi wa Ndebwe wilaya ya Chamwino, Said Lusogo (dereva wa basi), Omari Mkubwa (kondakta wa basi) na Mikdadi Zuberi ambaye alikuwa ni utingo wa lori.
Wengine ni Justin Makasi, Gabriel Chiwipe, Marick Masawe na Melina Maliseli, Wilson Sudai (wote wakazi wa Mpwapwa) watu wawili walitambulika kwa jina moja ambao ni Christina (Mpwapwa) na Nasibu mkazi wa Kongwa.
Ilielezwa kuwa amu zilikuwa zimetapakaa katika sehemu kubwa ya barabara ilikotokea ajali hiyo na kwamba magari hayo yalikuwa yameharibika vibaya sehemu za mbele. Kadhalika baadhi ya mabomba yaliyokuwa kwenye lori yalikuwa yamerushwa umbali wa karibu meta 20 kutoka eneo la ajali.
Mashuhuda walisema Polisi wa Kituo cha Kongwa walifika katika eneo la ajali muda mfupi tu baada ya magari hayo kugongana na kwamba walisaidia kudhibiti usalama wa mali za abiria, zikiwamo simu za mkononi zaidi ya 20 ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa polisi Mkoa wa Dodoma.
Mashuhuda wazungumza
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza kufika katika eneo la tukio, alisema chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni uzembe uliofanywa na dereva wa lori ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Watu wote niliowahoji walimtaja dereva wa lori kuwa ndiyo chanzo na hata ukiangalia mwenyewe utaona jinsi alivyomfuata mwenzake katika eneo lake, hali ni mbaya sana,” alisema Kangoye.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mpwapwa, Dickson Kimaro alisema dereva wa lori alikuwa akitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake, ndipo ghafla akakutana uso kwa uso na basi.
Kimaro alisema wilaya ya Kongwa mbali na kupokea miili ya marehemu, ilifanya juhudi za kupeleka timu ya waganga pamoja na magari ya kubeba majeruhi ambao waliwahishwa katika hospitali ya Kongwa na wengine Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mmoja wa majeruhi, Safari Balaigwa alisema kuwa walikuwa katika mwendo wa kawaida lakini ghafla waliona lori likija mbele yao na kugongana na basi uso kwa uso.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527