DKT SALIM AMSHANGAA RAIS KIKWETE


Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa bungeni kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu walikuwa wanampa taarifa kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua iliyofikia,” alisema Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake na anazingatia mambo mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21, mwaka huu Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani kutekelezeka. 
Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Serikali. Alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa na Tume na kuegemea katika muundo wa serikali mbili na idadi ya watu walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa ni ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na ubunge kama ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa kuwepo bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni pendekezo la mtu kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo huku akisema baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi ambayo hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali katika sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya chama chake ili aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba Mpya haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo limeingizwa siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza kuleta matatizo.
“Tuko katika hali ambayo si nzuri inayohitaji uongozi thabiti, viongozi wote watambue umuhimu wa zoezi hili kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho ndicho kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari masilahi ya Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili zinazoshindana kuhusu idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai kukaa pamoja na kumaliza tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila misuguano.
“Mwezi huu wa Julai ni muhimu sana, ni mwezi pekee uliobaki wa kuwaweka pamoja wanaotofautiana. Kila jitihada zinatakiwa kufanyika ili kuhakikisha Bunge Maalumu linakutana tena Agosti na wapinzani waliosusa wanarejea ili kumaliza kazi hiyo kabla ya kutoa rasimu ya tatu kwa ajili ya kura za maoni,” alisema na kuonya kuwa kuendelea na katiba ya sasa kunaweza kuleta matatizo.
Neno ‘wasaliti wa Mwalimu Nyerere’ lamchefua
Aidha, Dk Salim ameeleza kusikitishwa na kukatishwa tamaa na kauli za baadhi ya wanasiasa dhidi yake na wajumbe wenzake wa Tume kwa kuwaita wasaliti na hasa kitendo cha kutilia shaka uzalendo wao.
“Inakatisha tamaa sana. Mimi nina umri wa miaka 72, kati yake zaidi ya miaka 30 nimeitumikia nchi yangu, haiingii akilini katika umri huu wa mwisho nianze kuisaliti nchi yangu, inasikitisha sana kusikia eti hawa wasaliti wa Mwalimu Nyerere,” alisema.
Dk Salim ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere (MNF), alisisitiza kuwa wajumbe hao wamekuwa wakishutumiwa na watu wenye malengo yao, akitolea mfano kuwa hata Dk Mwesiga Baregu aliwahi kushutumiwa na chama chake na kutakiwa ajitoe kwenye tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Itakumbukwa kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikishutumiwa na wanasiasa hasa kutoka CCM kutokana na mapendekezo yake ya mfumo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mbili zinazoungwa mkono na chama hicho.
Kutokana na tofauti hiyo, wajumbe walio wengi wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka CCM waliamua kubadili baadhi ya vifungu vya rasimu.
“Ni bahati mbaya sana binadamu unapotukanwa, unatupiwa madongo, tunaonekana wapuuzi kwa kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, inaumiza sana,” alisema.
Kama ambavyo Jaji Warioba amesema mara nyingi, Dk Salim aliitetea Rasimu ya Katiba, akisema kilichopendekezwa ndiyo picha halisi ya maoni ya Watanzania.
Alisema Tume hiyo ilikusanya maoni ya wananchi yenye hoja nzito yakieleza hasa matatizo yao katika nyanja mbalimbali kama afya, elimu, ardhi na mengine, ingawa hoja kuhusu muundo wa Serikali ndizo zinaonekana kushikiwa bango na wanasiasa.
Alisema ushahidi wa watu waliohojiwa upo katika maandishi, sauti na picha za video na idadi yao inatosha kuwakilisha Watanzania wote.
“Wanasema hatukuhoji watu wengi, waliohojiwa ni representative sample (sampuli), huwezi kuhoji Watanzania wote milioni 45,” alisema Dk Salim.
Alisema ni jambo la kushangaza kuwa mchakato umetekwa nyara na wanasiasa lakini Katiba inastahili kuwa ya kitaifa ya Watanzania wote, wenye vyama na wasio na vyama vya siasa.

Alisema hata kwenye tume, walikuwapo wajumbe zaidi ya 12 ambao hawatokani na CCM, wakitoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na wote walikuwa na mawazo tofauti lakini waliamua kuyaweka kando na kutoa rasimu inayotoa taswira ya mawazo na masilahi ya wananchi.
Chanzo-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527