RC DAR ES SALAAM AKANUSHA TAARIFA ZA DC KUTISHIWA BAADA YA KUVUNJA DANGURO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amekanusha tuhuma zilizoandikwa  na gazeti moja la kila siku  kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke  Sophia Mjema ametishiwa maisha baada ya kuvunja danguro la Temeke.
 
Akizungumza ofisini kwake jana, Mkuu huyo wa Mkoa alisema gazeti hilo liliandika habari hiyo ambayo si ya kweli na kuongeza kuwa ina lengo la kudidimiza operesheni hiyo.
 
“Naomba niwatoe hofu habari hizo si za kweli na Mkuu wa Wilaya Sophia Mjema ametueleza kuwa si kweli na hivyo tunaamini mwandishi wa habari hiyo hana lengo zuri,” alisema Sadik.
 
Aliongeza kuwa danguro hilo lilikuwa ni kichaka cha wanawake wadogo wanaojihusisha na ngono, wavuta bangi  na dawa za kulevya.
 
“Kwa kweli kama kuna madanguro mengine tunaomba yafichuliwe ili wanaofanya biashara hizo waweze kuchukuliwa hatua za kisheria haraka na tunaahidi kuwa operesheni hii itakuwa endelevu,” alisema.
 

Aidha alitoa rai kwa wananchi ambao katika mitaa wanayoishi kuna madanguro watoe taarifa hizo haraka kwa vyombo vya usalama ili  hatua zichukuliwe mara moja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post