Aibu!!! VIKONGWE WAWILI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KULAWITI WATOTO 6 WA SHULE ZA MSINGI HUKO BUNDA

Wazee wawili akiwemo mlinzi mmoja wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya wilaya ya Bunda, mkoani Mara, wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kulawiti wanafunzi sita wa shule za msingi zilizoko wilayani Bunda.


Waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, ni pamoja na Thomas Machugu (72) ambaye ni mlinzi na mkazi wa mtaa wa Saranga.

Mwingine ni Salum Mfumbasi (66) ambaye ni mfanyakazi wa ndani kwa mfanyabiashara mmoja wa  mjini Bunda.

Watuhumiwa hao walifikishwa juzi katika mahakama hiyo mbele ya hakimu, James Manota na kusomewa mashitaka yao na mwendesha mashitaka wa polisi Masood Mohammed.

Akiwasomea mashitaka yao, Mohammed alisema washitakiwa hao wote kwa pamoja waliwalawiti wanafunzi hao, ambao umri wao ni kati ya miaka 10 na 13 kwa tarehe na muda tofauti, katika maeneo mbalimbali mjini hapa.

Alisema kuwa polisi waliwagundua watu hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema na kwamba baada ya kuwahoji watoto hao walisema kila kitu jinsi washitakiwa hao wamekuwa wakiwaingilia kwa zamu, pindi wanapokwenda shuleni baada ya kupita katika maeneo hayo.

Aidha, aliongeza kuwa baada ya watoto hao kupelekwa hospitalini na kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ilibainika kuwa walikuwa wamekwishaharibiwa sehemu zao za siri.


Washitakiwa wote kwa pamoja wamekana mashitaka yao na kupelekwa mahabusu hadi Mei 22 mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post