TANESCO KUSHIRIKIANA NA SUNGUSUNGU SHINYANGA VITA DHIDI YA WANAOHUJUMU MIUNDO MBINU YAKE

Afisa uhusiano na wateja TANESCO Mkoa wa Shinyanga bwana Amoni Michael akizungumza wakati wa kikao cha makamanda wa jeshi la jadi sungusungu
Shirika la umeme nchini TANESCO mkoa wa Shinyanga limeliomba Jeshi la jadi sungungu na wakazi wote wa  mkoa huo kushirikiana na shirika hilo katika kulinda miundo mbinu ya shirika hilo kwa  kuwafichua watu wote wanaohujumu miundombinu hiyo kama vile kuiba nyaya,mita,mafuta ya transfoma.

Wito huo umetolewa jana na afisa uhusiano na wateja TANESCO Mkoa wa Shinyanga bwana Amoni Michael wakati wa kikao cha makamanda wa jeshi la jadi sungusungu maarufu kwa jina la Sanjo kutoka katika wilaya ya Shinyanga vijijini,Shinyanga mjini na wilaya ya Kishapu kilichofanyika katika shule ya Msingi Kolandoto kata ya Kolandoto katika manispaa ya Shinyanga.

Afisa huyo wa TANESCO aliwataka Sungusungu kusaidiana na shirika hilo pamoja wananchi kuwabaini wanaohujumu miundo mbinu kama vile mita,transimita,nguzo na nyaya kwani panapotokea uhujumu kuna athari kubwa kiuchumi na kijamii kwani asilimia kubwa vitu vingi vinatumia umeme hivyo kama hakuna umeme hata ghrama za maisha zinapanda.

Alisema ni vyema wananchi wakashiriki katika ulinzi wa miundombinu ya umeme huku akiwatahadharisha wanaolima katika eneo la njia ya umeme kuacha kufanya shughuli za kiuchumi kwani wanaweza kupata matatizo ikiwemo kupoteza maisha kutokana na wananchi wasio waaminifu kuharibu miundombinu ya umeme.

Naye mhandisi wa njia kuu za umeme mkoa wa Shinyanga Job Bidya alisema serikali na TANESCO zinapata hasara kubwa pindi miundombinu inapohujumiwa  hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za shirika hilo katika kuzalisha,kusafirisha na kusamabaza umeme kwa wateja wake.


 Bidya alisema TANESCO itatoa zawadi kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa sahihi kuhusu wanaohujumu miundombinu.

Nao viongozi wa sungungu walisema watatoa ushirikiano kwa mamlaka mbalimbali kama vile  za umeme,maji,reli,barabara na simu katika kulinda miundo mbinu yao kwani hasara zinazotokana na kuharibu miundombinu hiyo zinawaathiri wananchi wote ndiyo maana wakaamua kuitisha kikao na mamlaka hizo ili kuangalia namna ya kupambana na wanaohujumu miundombinu hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post