DIWANI NA MTENDAJI WA KATA WAIBA PESA ZA WATOTO YATIMA HUKO GEITA



 
Wananchi katika kata ya Isulwa Butundwe wilayani Geita mkoani Geita wametishia kuifunga ofisi ya mtendaji wa kata hiyo Sadik Masalu kwa tuhuma ya kutumia pesa za watoto wanaoishi mazingira magumu kwa matumizi yao binafsi.

 Afisa mtendaji huyo anadaiwa kushirikiana na diwani wa kata hiyo kupitia CCM James Maweda kutumia kwa matumizi yao binafsi shilingi milioni moja na laki 8 pesa za watoto yatima zilizotengwa kwa ajili ya kuwasomesha.

Wakiongea kwa nyakati tofauti jana wananchi hao walisema kuwa shilingi laki nane zilitolewa na halmashauri ya wilaya ya Geita kwa ajili ya kusomesha watoto wenye mazingira magumu wanatoka kata hiyo.

Waliongeza kuwa  shilingi milioni moja ni marejesho ya asilimia ishirini ya mapato yanayorudishwa katani kutokana na mapato yanayokusanywa kwa ajili ya maendeleo ya kata na zote zimetumiwa na viongozi hao kwa matumizi yao binafsi.

Aidha walisema kuwa mara baada ya kusubiri kwa muda mrefu kuwa watoto wenye mazingira magumu wataenda shuleni lakini haikuwa hivyo na baada ya kufuatilia wakagundua kuwa mtendaji huyo alienda kuzichukua benki ya NMB tawi la Geita.

Walifafanua kuwa  baada ya kuchukua pesa hizo alizifanyia matumizi yake binafsi na kukaa kimya bila kutoa taarifa kwa wananchi huku diwani wa kata hiyo akishirikiana naye.

Viongozi hao walipobanwa zaidi mbele ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri walikiri kwa pamoja na kupewa muda wa mwezi mmoja wawe wamerudisha pesa hizo.

Hata hivyo pamoja na kupewa mwezi mzima  jambo la kushangaza mwezi umeisha na hawajarudisha na hawajachukuliwa hatua.

Mtendaji wa kata hiyo Sadik Masalu alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa ni kweli alizichukua pesa hizo lakini kwa sababu alikuwa na matatizo ya kifamilia akapeleka watoto wake shuleni.

 “Kwa kweli nilizitumia na hata baada ya kikao kilipokuja cha kunijadili nilikiri na kuomba wanipe muda wa kuzirudisha mbele ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya”,alisema.

Naye diwani wa kata hiyo James Maweda alisema  yeye hahusiki na tuhuma hizo isipokuwa mtendaji wa kata ndiyo alizichukua pesa hizo na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi na ameshapewa muda wa mwezi mmoja azirudishe.

Kwa upande wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Geita Ali Kidwaka alipoulizwa kuwa ni hatua gani alizozichukua dhidi ya ubadhilifu huo alisema kuwa taarifa hizo anazo na anazidi kuzifuatilia  kwa kuchunguza zaidi hususani kwa mtumishi wake ambaye ni mtendaji wa kata Sadik Masalu.

Hata hivyo aliongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika wa ubadhilifu wa fedha hizo.

Na Valence Robert -Geita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post