Majanga!! WAKOMAA KUMWOMBEA MAREHEMU ILI AFUFUKE,WADAI KAFA KWA KULOGWA







Ndugu wa marehemu Elitha Kaizilege wakipeleka mwili wa ndugu yao kanisani kwa ajili ya maombi.


HIKI ni kioja! Ndugu wa marehemu Elitha Kaizilege ambaye alipatwa na mauti katika Hospitali ya Kairuki iliyopo Mikocheni jijini Dar wiki iliyopita, walifanya tukio la aina yake baada kutokukubali kama ndugu yao amefariki.


Ndugu hao wa marehemu walizuia mwili huo kupelekwa mochwari na badala yake wakauombea kwa saa sita hospitalini hapo wakiamini ataamka, kwani ugonjwa wake ni wa kulogwa.

Kana kwamba haitoshi, baada ya muda huo kupita, ndugu hao, wanaosadikika kuwa ni waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Mchungaji Josephat Gwajima, waliupeleka kanisani hapo ambapo uliombewa zaidi ya saa mbili mwili huo ili uamke, ikashindikana.


Kwa mujibu wa chanzo chetu, marehemu ambaye alirejea nchini hivi karibuni kutoka Marekani alikoenda kuhudhuria mahafali ya mwanaye anayesoma nchini humo, alianza kuumwa kimasihara, hasa kwa vile ugonjwa wake ulikuwa haueleweki licha ya kupelekwa katika hospitali mbalimbali jijini.

Wakati akiumwa, inadaiwa kuwa tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua ni sikio lakini katika vipimo kadhaa alivyopimwa, havikuonyesha ugonjwa.

Kwa mara ya mwisho kuna madai kuwa alikuwa na kansa ya kichwa, kitu ambacho pia kiliwashangaza ndugu ambao walishangaa ni wapi alipoutoa ugonjwa huo mara moja.
Inadaiwa pia kuwa wakati akiumwa, mama huyo aliwahi kupigiwa simu na mtu anayehisiwa ni mganga wa kienyeji kutoka Kigoma, ambaye haikufahamika walichoongea.

Inasemekana kuwa mara tu baada ya madaktari wa Hospitali ya Kairuki kuwataarifu kuhusu kifo cha mgonjwa wao, walizuia mwili huo kupelekwa chumba cha maiti wakiamini hajafariki, na kwamba wanataka wafanye maombi ili kumfufua.

Baada ya maombi ya hospitalini na kanisani kushindikana, mchungaji aliyeongoza ibada hiyo, ambaye jina lake halikuweza kujulikana mara moja, aliwaambia ndugu hao kuwa marehemu hataweza kuamka na kuwataka waupeleke mwili huo chumba cha kuhifadhia maiti.

Waandishi wetu walimtafuta kiongozi mkuu wa kanisa hilo mchungaji Josephat Gwajima ili aweze kuzungumzia suala hilo, lakini waliambiwa kuwa yuko Japan kwa kazi ya kuhubiri neno.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi waandamizi wa kanisa hilo, aliyekataa jina lake kutajwa , alisema maombi ya aina hiyo hufanyika kanisani hapo na mara kadhaa, watu waliodhaniwa wamefariki waliweza kuinuka.

Haruni Sanchawa na Gabriel Ng’osha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post