AKINA MAMA WAENDA KUJIFUNGUA NA MADUMU YA MAJI,ZAHANATI HAINA HUDUMA YA MAJI-SHINYANGA


Imeelezwa kuwa Zahanati ya kijiji cha  Singita kata ya


Usanda wilaya ya Shinyanga inakabiliwa na uhaba wa maji hali  inayowalazimu akina mama  wanaokwenda kujifungua  kwenda na maji yao ambapo wakati mwingine hulazimika kununua hayo yanaoyouzwa shilingi mia mbili kwa  dumu la lita  ishirini.

Wakiongea na waandishi wa habari waliotembelea zahanati hiyo akinamama walisema   wanapokwenda kujifungua  wamekuwa wakilazimika kununua maji kwa ajili ya kufulia nguo zao  na kuoga jambo ambalo limekuwa ni changamoto  kwao kwani wanatumia gharama kubwa  wakati  kipato chao ni kidogo.

Walisema mbali na Zahanati hiyo kukosa huduma ya maji lakini pia katika zahanati hiyo kuna ukosefu wa dawa wa  mara kwa mara,ukosefu wa maabara  na baadhi ya vifaa tiba na wamekuwa wakilazimika  kufuata vipimo vingine katika hospitali ya  mkoa  wa Shinyanga au kwenye maduka ya dawa ya  watu binafsi .

“Katika suala la maji tunatumia gharama  kununua dumu moja  shilingi 200  kwa kipindi hiki cha masika lakini msimu wa kiangazi maji huwa adimu tunalazimika kununua dumu moja mpaka shilingi 600 ili kuweza kuoga na kufua pindi tunapojifungua,isitoshe kuna uhaba wa dawa, maabara ya kupata vipimo vya magonjwa mengine kama kifua kikuu,kichocho na mengineyo”alisema  mkazi wa kijiji hicho Hawa John.

Kwa upande wake  muuguzi  wa zahanati  hiyo Leticia  Anthony alisema kuwa kweli Zahanati  inachangamoto ya uhaba wa maji hivyo hata wao hulazimika  kununua kwaajili ya matumizi ya usafi,pia akina mama hao wanapokuja kujifungua hulazimika kununua maji ya kuoga na kufulia dumu lenye lita ishirini shilingi 200.

“Kweli  zahanati hii haina maabara,vifaa tiba,vifaa vilivyopo ni kwa ajili ya upimaji malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) ikiwa wastani wagonjwa  kwa siku ni 60 hadi 70 zaidi ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano huja kwa maradhi ya malaria na wakubwa kwa maradhi ya kikohozi ambapo wanaokwenda kujifungua kwa mwezi hufikia zaidi ya 40”alisema Antony.

Naye ofisa  afya kata ya  Usanda  Mussa Chande  alisema kuwa Zahanati hiyo inahudumia vijiji vitano vya  Singita, Shagaluba,Manyada, Nzagaluba, na Igaganulwa na katika   kata nzima  kuna idadi ya watu zaidi ya 15,000


Diwani wa kata  hiyo Abeid Aljabir alikiri kuwepo kwa uhaba wa maji katika Zahanati hiyo  na kwamba  tayari kuna mabomba ya maji  ambayo tangu yawekwe hayajawahi kutoa maji hali ambayo imekuwa ikiwalazimu akinamama kununua maji huku akiiomba serikali kuwapatia maji kutoka mradi wa ziwa Victoria  ili kuondoa kero hiyo.

via>>Sungwakareny blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post