Siri Mauaji ya Vikongwe Shinyanga yafichuka iko hapa!!!! MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA AFUNGUKA MENGI,ADAI SIYO USHIRIKINA,ALIA NA VIJANA,SOMA HAPA





Aliyesimama ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anna rose Nyamubi,kushoto ni afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa Tanzania(UNIC) bi Usia Nkhoma Ledama
Kufuatia kuendelea kujitokeza kwa vitendo vya mauaji ya vikongwe (hususani akina bibi),Mkuu wa wilaya ya Shinyanga  Annarose Nyamubi ameonesha kukerwa na kusikitishwa na vitendo hivyo dhidi ya wazee na kusema kuwa sababu kubwa inayosababisha kuendelea kutokea kwa mauaji ya vikongwe hivi sasa katika mkoa wa Shinyanga ni urithi wa ardhi yakiwemo mashamba makubwa na mifugo wala siyo ushirikina kama wengi wanavyofikiria.



Mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga ndugu Nyamubi ameyasema hayo juzi mjini Shinyanga akiwa mgeni rasmi wakati wa warsha iliyoandaliwa na kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa Tanzania ambayo iliwakutanisha pamoja wanafunzi wa shule 10 za sekondari ikiwemo shule ya Uhuru,Buluba,Kizumbi,Chamaguha,Mazinge pamoja na vyuo vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga kama vile VETA,MUCCOBS na chuo cha Ualimu cha Shinynga kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu kazi mbalimbali za Umoja wa mataifa ikiwemo malengo ya millenia hapa nchini kama vile haki za binadamu,afya ya uzazi na elimu kwa watoto.

Nyamubi alisema Mkoa wa Shinyanga bado unakabiliwa na changamoto ya mauaji ya vikongwe na hali hiyo inaonekana kuwa ndiyo  sifa ya mkoa na kuongeza kuwa mauaji hayo hivi sasa hayatokani na uchawi wala imani za kishirikina bali mauaji hayo yanatokana na wanafamilia kugombania mali za urithi katika jamii.
“Vijana tumieni ujana wenu kuleta mabadiliko,hasa katika suala hili la mauaji ya bibi zetu,niwaambie ukweli kwamba sababu kubwa ya mauaji ya bibi zetu leo hii siyo ushirikina,bali sababu kubwa ni suala la ardhi kwa maana ya mashamba makubwa na mifugo”,alieleza Nyamubi.

“Tumebaini kuwa hawa bibi zetu wanaolengwa kuuawa ni wale ambao waume zao walishafariki dunia,na kwa mila tulizonazo wao ndiyo warithi wa mali hizo na katika hilo bibi hao wanasahau kuwa wana watoto wakubwa wa kiume tena wameoa ambao nao wanazitolea macho mali zile zile halafu bibi zetu wana kitu kimoja,huwa wanachagua mjukuu mmoja wanakuwa karibu nao,ndiyo wanaanza kuwarithisha mali hali ambayo inaleta chuki kati ya bibi,watoto na wajukuu”,aliongeza Nyamubi.

Alifafanua kuwa kufuatia chuki inayotokana na nani arithi mali hizo ndipo wale watoto wanaanza kutengeneza mipango ya kumuua bibi huyo ambapo kuna watu maalum wanaolipwa pesa kwa ajili ya kutekeleza mauaji kwa kutumia mapanga na sasa wamebuni mbinu nyingine ya kutumia aina flani na vishoka vidogo wanawapiga vikongwe sehemu za uti wa mgongo ili wafe bila kupiga kelele.

“Wahusika wakuu wa mauaji ya vikongwe ni watoto,tukiwakamata wanasema,sisi tumepata hata uthibitisho kutoka kwa waganga wa kienyeji wanasema,wale watoto waliolipia wauaji kutokana na hofu ya kuua huwa wanakwenda kuoshwa ili kuondoa laana ya kuua wazazi wao”,alisema Nyamubi.

Kufuatia hali hiyo aliwataka vijana wa Shinyanga kujadili kwa kina katika kuondokana na mauaji hayo na kwamba watumie fursa mbalimbali zinazotolewa na Umoja wa mataifa ikiwemo kutumia miradi ya umoja huo kupiga vita mauaji hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanywa na ndugu wa karibu katika jamii lakini wakumbuke kuwa vijana wa leo ndiyo vikongwe wa kesho hivyo hali inaweza kuwarudia wao.

“Katika mambo muhimu ya kuzungumzwa na kupigwa vita ni hili la mauaji ya bibi zetu,mauaji haya yanautia aibu mkoa wetu,wenye utajiri wa kila aina,na sasa viwanda vingi vinajengwa hapa na vingine vilishaanza kufanya kazi,kwanini vikongwe wauawe?,je nyinyi kama vijana mnafurahia hali hii?,simameni kidete kuielimisha jamii,na nyinyi pia mmbadilike fanyeni kazi msitegemee urithi wa mali kutoka kwa wazazi wenu,mauaji hayo mengi yanafanywa na vijana”,aliongeza Nyamubi.

Akizungumza katika warsha hiyo afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa Tanzania(UNIC) bi Usia Nkhoma Ledama alisema lengo la Umoja wa mataifa kukutana na wanafunzi wa  shule za sekondari na vyuo mkoani Shinyanga ni kuwahamasisha vijana ili wajue kazi zizazofanywa na Umoja wa mataifa lakini pia kuwaelimisha fursa za umoja huo kwa vijana hivyo kuwaunganisha watu wa chini na umoja huo.

Aidha afisa habari huyo aliwataka vijana waliopo shuleni na vyuoni kutumia fursa zinazotolewa na Umoja wa mataifa ili kuleta mabadiliko katika jamii ikiwa ni pamoja na kupigania haki za binadamu,afya ya uzazi,amani  na kuwa wajasiriamali ili kuondokana hali ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

Katika hatua nyingine Ledama alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi na walezi wa wanafunzi kufuatilia mienendo ya wanafunzi wao na kuwasaidia kwani elimu ndiyo njia pekee ya kuondoa umaskini katika jamii huku akiwataka vijana kuachana na ngono ili watimize ndoto zao na kujifunza kuwa wajasiriamali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments