RAIS KIKWETE ATUMA SALAM ZA RAMBI RAMBI KIFO CHA MKUU WA MKOA WA MARA

Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa (aliyeshika karatasi)
Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Gabriel Tuppa (aliyeshika karatasi) enzi za uhai wake

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa  na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  Mhe. Hawa A. Ghasia kufuatia kifo cha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. John Gabriel Tuppa, aliyefariki  tarehe 25 Machi, 2014 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
Pokea rambirambi zangu za dhati na  masikitiko makubwa kufuatia   kifo cha Mhe. John Gabriel Tuppa. Ni huzuni kubwa na pigo kwa Serikali na hasa kwa Watendaji wenzake mkoani Mara ambao alikuwa akifanya nao kazi.
Marehemu John Gabriel Tuppa amefariki  tarehe 25 Machi,2014 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.Rais pia amemwomba Mhe. Ghasia amfikishie salamu za pole kwa Mke  wa Marehemu,Watoto na Familia ya Marehemu kwa kuondokewa na kipenzi chao. Rais amesema, anaelewa machungu wanayoyapitia katika kipindi hiki kigumu kwani wamepoteza nguzo imara waliyokuwa wakiitegemea katika maisha yao.“Hakika tumempoteza kiongozi mchapakazi ambaye amekuwa akijituma  na kuwatumikia Wananchi wake hadi dakika za mwisho za uhai wake.  Pengo aliloliacha Marehemu Tupa haliwezi kuzibika kamwe lakini hatuna budi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu kuipumzisha roho ya Marehemu mahali pema peponi” Amina.Taratibu na maandalizi ya mazishi zinafanywa kwa ushirikiano wa Familia, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI.
Marehemu Tupa alizaliwa tarehe 01 Januari, 1950 na katika enzi za uhai wake amewahi kuongoza Wilaya za  Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mwaka 2011. Ameacha Mke na watoto watano.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

25 Machi,2014

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post