MWANAFUNZI WA DARASA LA NNE ABAKWA KWENYE UCHOCHORO,KESI YADAIWA KUMALIZWA KIFAMILIA

WAKATI asasi na taasisi mbali mbali zikiwemo TGNP, TAMWA na WRP zikipinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, hali hiyo imeonekana kutopewa mwitikio na baadhi ya familia.

Kutopewa kwa kipaumbele na kushindwa kuwachukulia hatua wanaofanya vitendo  hivyo kumetokana na Familia moja jijini Mbeya kutaka kumaliza kifamilia suala la ubakaji lililotokea hivi karibuni.

Tukio hilo lilitokea Machi 13 mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika Mtaa wa Mapambano Kata ya Iyela wakati mtoto wa kike alipotumwa dukani na Mama yake Mzazi na kukumbwa na tukio hilo.

Mtuhumiwa wa tukio hilo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Iyela Jijini Mbeya Patrick Ndelwa(18) anatuhumiwa kumbaka Mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka nane(jina limehifadhiwa) shule ya Msingi Mapambano Jijini Mbeya.

Hatua ya kufikia wazazi wa pande zote mbili kutaka kumalizana kifamilia imetokea baada ya Jeshi la Polisi kushindwa kufungua jalada la tukio hilo  tangu  Machi 14, mwaka huu lilipolipotiwa.

Aidha jalada la tukio hilo lilifunguliwa Machi 24 mwaka huu huku Polisi wakitaka yafanyike mazungumzo katika pande hizo mbili na kushindwa kuwachukulia hatua waliotenda makosa kama hayo.

Uchunguzi umebaini kufanyika kikao Machi 26,mwaka huu eneo la Mapambano Iyela kilichowakutanisha pande hizo mbili kwa nia ya kulimaliza nyumbani suala hilo huku upande wa mtuhumiwa ukidai kuwa aliyetenda kosa hilo ni yatima.

Aidha imebainika kuwepo kwa mkakati wa kumhamisha mwathirika wa tukio hilo kumpeleka Jijini Dar es Salaam kwa nia ya kupoteza ushahidi na Jalada kutopelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali ili kukwamisha taratibu za kumfikisha mtuhumiwa Mahakamani ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mama Mzazi wa mwathirika wa tukio hilo,Salome Msigwa alisema aligundua kubakwa kwa mwanae alipoanza kumuogesha Machi 13 mwaka huu majira ya saa kumi na mbili jioni na alipomuuliza alijibiwa kuwa aliyembaka ni Patrick Ndelwa ambapo alimtendea unyama huo katika kichochoro karibu ya nyumba yao.

Alisema baada ya kugundua tatizo la mtoto, alitoa taarifa kituo cha Polisi ambapo mtuhumiwa alikamatwa na mtoto kupelekwa kupimwa Hospitali ya Rufaa na kupewa Matibabu huku akitakiwa kufuatilia vipimo vingine Machi 28.


Baadhi ya wadau wamelalamikia kuongezeka kwa vitendo ya ukatili dhidi ya watoto na kwamba vimekuwa vikiongezeka Jijini Mbeya sehemu kubwa imekuwa ikichangiwa na Dawati la Kijinsia la Jeshi la Polisi kutokana na kugeuka Mahakama kuyamaliza matatizo kwa kupatanisha pande zinazotuhumiana.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amekiri kupokea tatizo hilo kwamba jeshi lake linafanyia uchunguzi suala hilo likikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.


Na Mbeya yetu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post